08/08/2025
KIMATAIFA
SOMA JINSI ISRAEL ILIVYOANZISHWA NA KWANINI HAIISHI KUPIGANA NA JIRANI ZAKE
Zaidi na zaidi ya watu na mataifa mbalimbali duniani wameendelea kuchefukwa na ukatili unaofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Ufaransa, Uingereza na Canada yamekuwa mataifa ya hivi karibuni kutangaza mpango wa kulitambua taifa la Palestina, ikiwa ni sehemu ya kuchoshwa na vitendo vya Israel dhidi ya Wapalestina.
Lakini kuelewa namna Israel ilivyoanzishwa, kunaweza kusaidia kwa sehemu kuelewa kwanini taifa hilo haliishi kuwafanyia Wapalestina vitendo vya kikatili, na kwanini ni ngumu kwa Israel kuishi kwa amani na majirani zake.
Maeneo matatu muhimu yanayofahamika leo hii k**a Ukingo wa Magharibi, Israel na Gaza – kwa pamoja yalijulikana k**a Palestina, na yalikuwa chini ya himaya ya Ottoman.
MASWALI MUHIMU
★Kwanini Israel na Palestina zinazozana
★Kwa nini Israel na Palestina zinapigania bonde la Jordan
★Jinsi Israel ilivyoundwa
Lakini himaya hii – iliyokuwa ikitawala eneo kubwa la ukanda huo - ilishindwa katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914-1918), na Muingereza akalichukua eneo hilo.
Ushindi huu wa Uingereza ulitokana na msaada mkubwa wa viongozi kadhaa wa Kiarabu wa eneo hilo waliokuwa wakitaka uhuru pia kutoka kwa himaya hiyo ya Ottoman. Uingereza iliwaahidi viongozi hawa kwamba k**a wakiisaidia kushinda, basi itawapa kutengeneza nchi ya umoja wa Kiarabu katika eneo hilo.
Wakati huu, idadi kubwa ya wakaazi wa eneo hilo walikuwa Waarabu, ikifuatiwa na idadi ndogo ya Wayahudi, na idadi nyingine ndogo zaidi ya watu wa asili nyingine mbalimbali.
Lakini ghafla, mwaka 1917, Uingereza ikatoa tamko la kuanzisha taifa ya Wayahudi ndani ya ardhi hiyo ya Palestina – ambayo idadi kubwa ya wakazi walikuwa Waarabu. Tamko hili linajulikana k**a Balfour Declaration.
Moja ya sababu ya Uingereza kutaka kufanya hivi, ilikuwa kutafuta uungwaji mkono wa Wayahudi katika maslahi yake na vita nyingine iliyotaka kupigana hapo Mashariki ya Kati.
Uamuzi huu ulizua mgogoro mkubwa kati ya Wayahudi na Waarabu na Waarabu dhidi ya Uingereza. Kumbuka, japo Wayahudi walikuwa na uhusiano wa kihistoria na ardhi hii, Waarabu pia walikuwa wameikalia ardhi hiyo kwa karne nyingi.
Pamoja na Uingereza kusisitiza kwamba haki za Waarabu waliokuwa wengi zitaheshimiwa, Waarabu waliendelea kupinga mpango huu wa kuanzisha taifa la Wayahudi ndani ya eneo lililo na Waarabu wengi.
Mgogoro huu ukazua vikundi vya wapiganaji wa Kiyahudi, waliokuwa wakitetea tamko la Muingereza kuanzisha taifa lao hapo Palestina, na vikundi vya wapiganaji vya Kiarabu vilivyokuwa vikipinga mpango huu wa Muingereza kutengeneza taifa la Wayahudi ndani ya ardhi yao.
MGOGORO KATI YA WAARABU NA WAYAHUDI
Kwa miaka mitatu hadi mwaka 1920, eneo hilo la Palestina likawa na mapigano makali sana kati ya Waarabu na Wayahudi, huku Waingereza wakiwa upande wa Wayahudi kuwasaidia kuwadhibiti Waarabu.
Ndani ya miaka ishirini baadae, pakatokea miminiko kubwa la wahamiaji wa Kiyahudi zaidi ya Laki moja (100,000) wakiingia katika eneo hilo la Palestina kutoka pande zote za dunia. Ongezeko hili kubwa la wahamiaji lilisababishwa pia na mateso waliyokuwa wakifanyiwa Wayahudi na WaNazi huko Ulaya
Unaweza kusema kwamba Wayahudi waliokuwa wakiishi Ulaya kwa upande mmoja wakawa wanakimbia mateso ya WaNazi na kwa upande mwingine wakaja kuongeza nguvu ya kupigania fursa ya kuanzishwa kwa taifa lao hapo Palestina.
Kufikia mwaka 1938, wakati vuguvugu la Vita ya Pili ya Dunia huko Ulaya lilikuwa limeanza pia. Uingereza ikaanza kutafuta kuungwa mkono na nchi za Kiarabu katika vita vyake huko Ulaya. Lakini hizihizi nchi za Kiarabu ndizo zilizokuwa zinapinga mpango wa Uingereza wa kuanzishwa kwa taifa la Wayahudi hapo Palestina.
Ili kuzipendezesha nchi za Kiarabu, hasa Misri na Saudia iliyokuwa na mafuta mengi, katikati ya mwaka 1939, Uingereza ikaweka katazo la kuingia zaidi kwa wahamiaji wa Kiyahudi hapo Palestina.
Katazo hili likawa k**a ndio limewachochea zaidi Wayahudi kupigania kuanzishwa taifa lao. Hapo Wayahudi waliokuwa wakiwaunga mkono Waingereza kuanzishwa taifa lao wakaungana na wengine wenye misimamo mikali, kuanzisha harakati za kijeshi ili kumuondoa kabisa Muingereza katika ardhi hiyo ya Palestina.
Mauwaji ya Wayahudi takribani milioni sita huko Ulaya, ikawachochea pia Wayahudi kuondoka Ulaya, na kuja kupigania kuanzishwa kwa taifa lao k**a walivyoahidiwa na Uingereza. Hadi kufikia mwaka 1947, tayari palikuwa na Wayahudi 630,000 katika ardhi ya Palestina.
Wakati huu, machafuko yalikuwa makubwa sana Palestina hadi Uingereza ikaongeza vikosi vya askari na wanajeshi wapatao 17,000 kutoka Uingereza. Kwa upande mmoja, Wayahudi na Wapalestina wanapigana, kwa upande mwingine Wayahudi wanavishambulia vikosi vya Uingereza ili kuwafukuza.
Kura ya kuigawanya Palestina
Baada ya machafuko hayo kuongezeka zaidi na Uingereza kushindwa kuyadhibiti, mwaka 1947, Umoja wa Mataifa ulipiga kura kuigawanya Palestina iwe na mataifa mawili; moja la Wayahudi na lingine la Wapalestina, na kuamua kwamba Jerusalem litakuwa jiji la kimataifa likitumiwa na mataifa yote haya mawili.
Karibu nchi zote za Kiarabu ziliukataa mpango huu. Zilihoji kwanini Wayahudi wapewe ardhi kubwa au sawa na ya Waarabu wakati idadi yao ilikuwa ndogo tu.
Uingereza – ambaye ndio mwanzilishi wa mgogoro wote huu – Ikakaa pembeni, na haikupiga kura katika mpango huo wa Umoja wa Mataifa. Ilipofika tarehe 14 Mei 1948, ikaondoka Palestina na kuwaachia tatizo hilo Umoja wa Mataifa.
Lakini saa chache tu kabla ya Uingereza kuondoka, Wayahudi wakatangaza taifa lao na kuliita Israel. Mwaka uliofuata, Umoja wa Mataifa ukalitambua taifa hili, na huo ndio ukawa mwanzo wa taifa la Israel k**a tunavyolifahamu leo hii.
VITA VYA SIKU SITA KATI YA NCHI ZA KIARABU NA ISRAEL
Vita vya siku sita kati ya mataifa matano ya Kiarabu dhidi ya Israel
Siku moja baada ya Israel kujitangazia uhuru, ilishambuliwa na kuzungukwa na mataifa matano ya kiarabu. Israel wakaitambua hii k**a ndio vita yao ya uhuru.
Kufikia mwaka 1949, Israel ilikuwa tayari inadhibiti eneo kubwa la ardhi hiyo ya Palestina.
Hii ndio vita iliyokuja kuchora ramani mpya ya eneo hilo la Palestina na kupatikana kwa vipande vinne muhimu vya eneo hilo. Makubaliano ya baada ya vita yakaipa Misri kushikilia Ukanda wa Gaza, Jordan ishikilie Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, na Israel ishikilie Jerusalem ya Magharibi.
Kutokana na vita hii, takriban Wapalestina 750,000 walikimbia au walifurushwa kutoka kwenye nyumba zao katika ardhi iliyokuja kuwa Israel, na wakaishia kuwa wakimbizi katika nchi zingine za Kiarabu. Tukio hilo linajulikana kwa Kiarabu k**a Nakba (Janga).
Kwa upande mwingine, mamia ya maelfu ya Wayahudi waliondoka, au walifukuzwa, kutoka nchi zenye Waislamu wengi katika Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, na wengi wao walielekea Israel, taifa jipya lililokuwa limezaliwa kwa nguvu.
Tangu wakati huo, kwa upande mmoja, Wayahudi wameendelea kupigana kuongeza kumiliki ardhi zaidi katika maeneo ambayo bado yanakaliwa na Wapalestina.
Kwa upande mwingine, Waarabu wamekuwa wakipigana kuwadhibiti Wayahudi kutowapora zaidi maeneo yao, lakini pia kurudi katika ardhi ya mababu zao ambayo Israel iliichukua kwa nguvu baada ya Uingereza kutambulisha wazo la kuanzishwa kwa taifa la Wayahudi katika ardhi ya Palestina.
Chanzo: (BBC).
Picha si halisi.
Sisi ni Lemera News