07/04/2026
“Usiwape watu vitu sana, maana watu wana watu wao.”
Maneno haya yamenigusa sana. Nimeyatafakari kwa kina na kwa undani mkubwa.
Watu wengi wenye roho nzuri hujikuta wakiingia dosari kwa sababu ya kuishi na matarajio, wakichezea k**ari imani zao mbele ya watu ambao hawana uhakika k**a wanathaminiwa mioyoni mwao, au k**a watapewa thamani sawa kwa wema wanaoutoa.
Umewahi kumpa mtu kitu kwa mapenzi ya dhati, akakifurahia, akakitumia, na kikamsaidia kweli? Nafsi yako hujisikiaje wakati huo? Moyo hujaa furaha ya aina gani?
Sasa jiulize, unapokuwa na matarajio ya mwitikio huo huo, halafu ukutane na kinyume chake, unajisikiaje?
Tunaambiwa mabaya hayasahauliki kirahisi, lakini wema mara nyingi husahaulika haraka, hasa kwa mtu asiyejali. Ndipo maana ya maneno haya inaonekana wazi zaidi:
“Usiwape watu vitu sana, maana watu wana watu wao.”
Yananifanya nitafakari: nimefanya mangapi? Na katika mizani ya kile nilichojifanyia na kile nilichowafanyia wengine, kipi kina uzito zaidi?
Katika maandiko ya dini tunaambiwa:
“Mpende jirani yako k**a unavyoipenda nafsi yako.”
Usiishie kwenye tafsiri ya juu, ingia kwenye maana yake.
Kuna sababu ya kuwepo kwa kipengele hiki: “k**a unavyoipenda nafsi yako.”
Hii inaonyesha wazi kuwa kujithamini ni msingi muhimu kabla ya kuwajali wengine. Lakini pia kuna mpaka, usizidishe hadi ukaangukia kwenye ubinafsi, uchoyo, umimi, au kuwatengea wengine. Usijitosheleze kupitiliza hadi ukajenga kiburi.
Wema una mipaka.
Haupimwi kwa hisia, bali kwa busara, subira, na muongozo wa imani.
Kuwafanyia sana watu huku ukijisahau wewe mwenyewe ni mwanzo wa kuvunja misingi inayoshikilia wema wako. Kwa sababu, hata ufanye mema mara ngapi, ukweli ni kwamba watu wengi husahau haraka.
Na siku ukikosea hata kidogo tu, utashangaa makosa hayo yakikuzwa, yakisimuliwa, na kurudiwa hadi ujute kwa nini uliwahi kuwa mwema kwa kiwango kile.
Wapo wanaosema: “Tenda wema nenda zako.”
Lakini ukweli ni kwamba si rahisi hivyo.
Moyo wa binadamu una pande mbili, hisia na maumbile. Unaweza kujilazimisha kupotezea maumivu, lakini ipo siku utamfanyia mtu unayemjali jambo la dhati, halafu akakuudhi kiasi kwamba msemo huo utauona k**a picha ya pesa kwenye gazeti lilofungiwa maandazi.
Na hapo ndipo utatambua, kuwa hata wema unahitaji mipaka.