07/02/2025
Mtangazi Mkongwe Leonard Mambo Mbotela,amefariki dunia leo tarehe 7 Februari 2025, asubuhi, akiwa na umri wa miaka 84.
Mbotela alizaliwa mwaka 1940 katika eneo la Freretown, Mombasa, na alikuwa mtoto wa kwanza kati ya watoto wanane wa James na Aida Mbotela.
Alianza kazi yake ya utangazaji mwaka 1964 katika Sauti ya Kenya (sasa Kenya Broadcasting Corporation - KBC) na alijulikana sana kwa kipindi chake maarufu cha "Je, Huu ni Ungwana?" ambacho kilianza kurushwa hewani mwaka 1966 na kuendelea kwa zaidi ya miaka 55.
Alikuwa mtangazaji hodari wa mpira hasa enzi za wachezaji k**a vile golikipa maarufu Mahmoud Abbas aliyembandika jina Kenya 1.
Leonard Mambo pia anajulikana sana kufuatia jaribio la wanajeshi kupindua serikali mwaka wa 1982 akiwa mtangazaji wa zamu siku hiyo.
Katika maisha yake ya kibinafsi, Mbotela alioa Alice Mwikali mwaka 1970, na pamoja walibarikiwa watoto watatu: Aida, Jimmy, na George.
Baada ya kustaafu aliendeleza tasnia yake ya uanahabari na pia kuimba katika vilabu tofauti tofauti jijini Nairobi.
Mbotela alistaafu rasmi mwaka 2022 baada ya kuhudumu katika tasnia ya utangazaji kwa miaka 58, na hivyo kuwa mtangazaji aliyedumu kwa muda mrefu zaidi nchini Kenya.
Kifo chake ni pigo kubwa kwa tasnia ya habari na utangazaji nchini Kenya, na mchango wake utaendelea kukumbukwa na kuthaminiwa na wengi.