11/09/2025
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za Vuli kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025, ikiwataka wananchi na mamlaka mbalimbali kujiandaa kwa changamoto na fursa zitakazotokana na mvua hizo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladslaus Changโa, alisema mvua za Vuli mwaka huu zinatarajiwa kuanza kwa nyakati tofauti kulingana na maeneo ya nchi, huku baadhi ya mikoa ikitarajiwa kupata mvua za wastani na mingine chini ya wastani.
Maeneo yatakayopata mvua
Kaskazini na Kati: Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara itaanza kupata mvua wiki ya pili ya Novemba 2025, zikitarajiwa kuisha Januari 2026. Hapa mvua zitakuwa za wastani hadi chini ya wastani.
Magharibi na Kaskazini-Magharibi: Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara na kaskazini mwa Kigoma inatarajiwa kuanza kupata mvua wiki ya pili ya Oktoba 2025. Mikoa ya Simiyu na Shinyanga itaanza wiki ya nne ya Oktoba. Mvua zitadumu hadi Januari 2026.
Pwani na Visiwa: Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, kaskazini mwa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba itapokea mvua kuanzia wiki ya pili ya Novemba hadi Januari 2026, ambazo pia zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani.
Dkt. Changโa amewataka wakulima kutumia taarifa hizo kupanga shughuli zao za kilimo kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu na kupanda mazao yanayofaa kwa hali ya hewa inayotarajiwa. Aidha, alisisitiza matumizi ya mbegu bora ili kuongeza tija.
Kwa upande wa wafugaji, alishauri kuandaa malisho na maji mapema, huku mamlaka za maji, nishati na miundombinu zikihimizwa kuchukua hatua za tahadhari ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.
โNi muhimu wananchi, kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa na kuchukua tahadhari stahiki. TMA itaendelea kutoa taarifa za mara kwa mara ili kuhakikisha usalama na ustawi wa jamii,โ alisema Dkt. Changโa.