10/06/2026
Waamini wa Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu Jimbo Kuu Katoliki Arusha wanaendelea kushiriki Kongamano maalum linalofanyika katika Parokia ya Roho Mtakatifu Ngarenaro, k**a sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa shirika hilo jimboni hapa.
Akiendelea na utoaji wa mada Padre Festus Mangwangwii, Paroko wa Parokia ya Moyo Safi wa Mama Bikira Maria Unga Limited, amewaasa wakristo na wanashirika kuchota neema katika fadhila za moyo Mtakatifu wa Yesu. Kwa njia hiyo,"msichoke kutenda mema,nyakati zote," alikazia.
Akijikita katika mada ya; “Kujitambua na kuwajibika kwangu kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu katika jamii kwa hali zote," amewataka wanamoyo na wakristo kwa ujumla kujikita katika maisha ya sala,upendo,umoja na mshik**ano katika jamii.
Kupitia mada hiyo, wakristo wanaalikwa kutambua wito wao na kuishi vyema maadili ya kikristo,kwani "Imani bila matendo,imekufa," alisisitiza Padri Festus.
Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu Jimboni Arusha, ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa neema na mafanikio ya shirika hili, pia nafasi kwa wanachama kuimarisha umoja, imani na dhamira ya kulitumikia Kanisa na jamii.
Semina hii ni mwendelezo kwa siku saba hadi Jumapili 13 June 2026 ambapo itatamatishwa na kilele cha Adhimisho la Misa ya Jubilei na kupokelewa kwa wanachama wapya katika Parokia ya Roho Mtakatifu Ngarenaro.
Sala:
Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu, fanya mioyo yetu ifanane na Moyo wako.