08/06/2026
π ARUSHA TANZANIA
AUWSA NA ROTARY CLUB WAKABIDHI VYOO VYA KISASA SHULE YA MSINGI LEVOLOSI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) kwa kushirikiana na Rotary Club pamoja na wadau wengine wa maendeleo, wamekabidhi rasmi mradi wa vyoo vya kisasa katika Shule ya Msingi Levolosi iliyopo Kata ya Levolosi, Jiji la Arusha, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya elimu na afya kwa wanafunzi.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika Juni 8, 2026, Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa AUWSA, Anne Mshana, alisema mamlaka hiyo imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutekeleza miradi ya usafi wa mazingira katika shule za msingi, ambapo zaidi ya vyoo 49 vinatarajiwa kujengwa katika maeneo tofauti ya jiji.
Alieleza kuwa mradi wa Shule ya Msingi Levolosi umehusisha ujenzi wa vyoo vyenye matundu 13 kwa ajili ya wasichana na wavulana, kwa gharama inayozidi shilingi milioni 50. Mradi huo unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wanafunzi 1,200 na kuchangia kuboresha hali ya usafi, afya pamoja na mazingira ya kujifunzia.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo walieleza kufurahishwa na kukamilika kwa mradi huo, wakisema miundombinu hiyo mpya itawasaidia kupata huduma bora za usafi na kuondoa changamoto zilizokuwepo awali kutokana na uchakavu wa vyoo vya zamani.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Levolosi, Abas Haji, aliipongeza AUWSA, Rotary Club na wadau wote walioshiriki kufanikisha mradi huo, akisema umeongeza thamani katika sekta ya elimu na ustawi wa wanafunzi.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuhamasisha ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha huduma muhimu za kijamii zinaimarishwa zaidi, huku akisisitiza umuhimu wa kujenga miundombinu jumuishi inayozingatia mahitaji ya watu wote, ikiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalum na watu wenye ulemavu.