16/11/2025
𝗕𝗔𝗥𝗔𝗭𝗔 𝗟𝗔 𝗠𝗔𝗔𝗦𝗞𝗢𝗙𝗨 (𝗧𝗘𝗖) 𝗠𝗡𝗔𝗧𝗨𝗞𝗢𝗦𝗘𝗔 𝗦𝗔𝗡𝗔 𝗪𝗔𝗞𝗔𝗧𝗢𝗟𝗜𝗞𝗜.
Tumsifu Yesu Kristo.
Jina langu ni Joseph Simon Mapunda, Muumini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga Mkoani Ruvuma ambaye kwa mapenzi ya Mungu mwaka jana 2024 nilikuja Dar es Salaam kikazi na naishi Tegeta.
Leo tarehe 15 Novemba, 2025 nimesoma andiko la Baraza la Maaskofu lililoitwa “Tafakari ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Juu ya Yaliyotokea Siku na Baada ya Uchaguzi-2025”
Awali ya yote kabisa naomba kuchukua nafasi hii kutoa pole za dhati kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wote waliopoteza ndugu zao katika vurugu zilizotokea tarehe 25 Oktoba, 2025 na siku zilizofuata wakati ambapo nchi yetu Tanzania ilijikuta katika matukio ambayo hayajawahi kutokea na hayafanani kabisa na utamaduni wa Watanzania. Matukio mageni haswa.
Naungana na Watanzania wote kuwaombea Marehemu wote wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka.
Napenda pia kuwapa pole wote waliopoteza mali zao, walipoteza biashara zao, walipoteza ajira zao na ambao wanapitia kipindi kigumu cha giza nene kutokana na kupoteza kipato ambacho kiliendesha maisha yao na familia zao ama wapendwa wao.
Kwa wale ambao wamehusika na uhuni huu ama kwa kuchochea ama kwa kutekeleza matukio ya uharibifu wa miundombinu ya umma, wizi wa mali za watu binafsi na umma, uchomaji moto wa majengo, magari na biashara za watu mbalimbali, Mwenyezi Mungu mwenye kutoa haki awape wanachostahili.
Naomba nirudi kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), bila kupepesa macho naomba kusema wazi nasikitishwa sana na mwenendo wa TEC kutoa matamko na maandiko ambayo badala ya kuponya Taifa yanachochea mgawanyiko, uhasama na kuligombanisha Kanisa na Serikali. Ni kweli Maaskofu ndio viongozi wakuu wa majimbo ya Kanisa Katoliki lakini ni muhimu Mababa Askofu mkaheshimu demokrasia na haki ya waumini wa Kanisa Katoliki kwa kutofanya mambo ambayo yanatokana na matakwa yenu, hayana baraka za waumini na yanawaharibia waumini wa Kanisa hili lenye heshima kubwa hapa Tanzania na ambalo limejengwa kwa jasho jingi la Watanzania vizazi na vizazi.
Nimeona mara kadhaa mnavyotoa matamko yenye vinasaba vya Kisiasa ambayo hakuna asiyejua kuwa yana mwelekeo wa siasa za upinzani na yanalenga kuishambulia Serikali. Sina tatizo na hoja mnazojenga lakini muhimu hapa kwa nini mnatumia Kanisa kufanya minyukano ya Kisiasa? Sisi Wakatoliki tumejenga Kanisa hili ili litupe huduma za kiroho, lihubiri Injili, lituweke pamoja na lidumishe amani na upendo kwa mwanadamu. Mnayoyafanya mnakiuka misingi hii.
Matukio yaliyotokea tarehe 29 Oktoba, 2025 na siku kadhaa za mbele hakuna yaliyemfurahisha, kwa nini nyie TEC mnaibuka na andiko la namna hii tena siku moja baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kutoa hotuba ya kuwaunganisha Watanzania, ya kuhimiza amani na utulivu, ya kujibu hoja za vijana na ya kuendeleza mkono wa maridhiano? Kwa nini Kanisa langu mnafanya mambo haya?
Tuseme Waumini wa Kanisa Katoliki na wanaopendezwa na mambo yanayoendelea nchini watawashangilia na kwa kuwa kuna kampeni ya mitandaoni ya kuitisha maandamano tarehe 9 Desemba, 2025 ili wajitokeze tena kupambana na vyombo vya dola k**a ilivyokuwa tarehe 29 Oktoba, 2025, mnataka watu wengine wauawe? hata wale ambao hawahusiki na uchochezi huu? Mnataka watu wengine waingie kwenye umasikini kwa biashara zao kuvamiwa, kuibiwa, kuharibiwa na kuchomewa moto? Au tuseme mnataka nchi iingie katika mapinduzi? Hamzijui gharama za mapinduzi?
Nimesoma andiko lenu mstari kwa mstari. Nataka niwaulize hoja chache kabisa na nyie mtafakari huku mkiongozwa na Roho Mtakatifu na roho wa haki;
1. Hivi Mababa Askofu kwenye andiko lenu mnasema tarehe 29 Oktoba, 2025 waandamaji walishambuliwa na kuuawa. Naomba kuuliza wale walikuwa waandamanaji au waleta vurugu, wezi na waharibifu wa mali za umma? Nyie mmetembea nchini nyingi Duniani, watu wanaoandamana huwa wanafanya vitendo ambavyo vilifanyika siku ile? Waandamaji wanakwenda kuwatia umasikini binadamu wenzao na kutishia maisha yao au wanakwenda kudai haki zao kwa watawala? Mababa Askofu mnafahamu kuwa hao mnaowaita waandamanaji walikuwa na silaha za moto na wameua askari polisi ambao walikuwa wanakabiliana nao walipokuwa wanakwenda kuvamia mali za watu kuvunja na kuiba? Mnafahamu hao watu wameua watu wasio na hatia wakijiita ni Askari?
2. Mababa Askofu mnajua kuwa hao mnaowaita waandamanaji walivamia vituo vya polisi ili kuchukua silaha na walipozikosa walivichoma moto vituo vya polisi vingi? mababa Askofu ina maana hamjuia madhara ya makundi ya wahuni kuchukua silaha na kuvamia watu na biashara zao? Mlitaka Askari wafanyeje? Nyie wenyewe nyumba zenu mmeweka Askari wenye silaha, leo watu waje kuvamia nyumba ya Askofu wachome moto na kisha waanze kutaka kuingia ndani hao Askari wenu watawaacha?
3. Mababa Askofu mnafahamu kuwa hao mnaowaita Waandamanaji walikwenda kuchoma moto jengo la Mawasiliano ambalo sio tu lingesababisha kuzimwa kwa mawasiliano yote bali nchi ingekosa mawasiliano kwa asilimia 100 kwa muda usiojulikana. Mnajua kuwa watu hao walishachoma eneo la mapokezi na jengo hilo liliokolewa na Askari Zimamoto waliowahi kabla ya moto kusambaa. Mnajua madhara ambayo yangetokea kwa nchi kukosa mawasiliano kabisa? Madhara kwa huduma za kifedha, mapato ya Serikali, huduma za matibabu hospitali, elimu na biashara zao watu.
4. Mababa Askofu mnafahamu kuwa hao mliowaita waandamanaji wamechoma moto vituo vya mafuta. Hamjui madhara ya kituo cha mafuta kikiungua hadi kufika hatua ya kulipuka?
5. Mababa Askofu mnahamu kuwa uharibifu wa miundombinu ya mwendokasi umesababisha huduma hiyo kusitishwa? Mnajua madhara yake? Kwa sababu nyie hamsafirii usafiri wa umma, mnatumia magari binafsi ambayo sisi waumini tumewanunulia.
6. Mababa Askofu mnafahamu kuwa vijana waliokuwa wanapambana kutafuta kipato wamefirisika na hivi sasa wanakosa mpaka pesa ya kununua chakula cha watoto wao majumbani kwa sababu hao mnaowaita waandamanaji wamewaibia na kuharibu kabisa biashara zao?
7. Mababa Askofu mnafahamu madhara mengine mengi ambayo k**a Nchi tunayapitia kutokana na vurugu zile?
Mababa Askofu hamuoni kuwa sio sawa kwa chombo hiki cha Dini, cha Kanisa Katoliki kubeba ajenda za chama cha upinzani ambacho kimeamua kutoshiriki uchaguzi ambao ni takwa la kikatiba ili kihamasishe watu kuleta vurugu ndani ya nchi? Kwani mkitoa tamko la kujenga imani za watu, watu kumrudia Mungu, kutubu na kujisahihisha pamoja kuhamasisha amani, upendo na utulivu mtapungukiwa nini?
Sawa, sasa mnatwambiaje Wakatoliki tujiandae kwa majambia, visu shoka, mawe na manati ili tukapambane na Polisi wenye silaha na JWTZ tarehe 9 Desemba, 2025 ili mje muandike tafakari nyingine ya TEC au mtatuletea bunduki, mabomu na mizinga ya kukabiliana na dola inayosimamia utawala wa Sheria?
Rais kaunda tume ya kuchunguza chanzo cha vurugu na kutoa mapendekezo ya namna ya kushughulikia mambo yaliyojitokeza tarehe 29 Oktoba, 2025 na nyie mmetoa tamko siku inayofuata, kwa hiyo mnataka sisi Wakatoliki tumsikilize Rais au tuwasikilize nyinyi TEC? Kwa nini mnataka kushindana na Rais? Hii nchi inaongozwa na TEC au inaongozwa na Serikali ambayo imewekwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi?
K**a na nyie TEC mnataka kuwa viongozi wa kisiasa kwa nini msiwe mnagombea nafasi za kisiasa k**a wanavyofanya viongozi wa madhehebu mengine ya Kikristo? Ili nanyi muwe na haki na mamlaka ya kiuwakilishi. Maana hivi mnavyofanya mnapaswa kuulizwa ni wananchi wanawatuma au mnajituma wenyewe?
Hamkuanza tabia hizi leo, mlifanya sana wakati wa tawala zilizopita. Hivi mmewahi kuwaza viongozi wa Serikali ambao ni Wakatoliki tena wengine ni wasaidizi wa karibu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnawaweka katika mazingira gani? Hebu vaeni viatu vya Makamu wa Rais Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye ni Mkatoliki, Wasaidizi katika Ofisi Binafsi ya Rais ambao ni Wakatoliki na wanakuja kusali kwenye Ibada ambazo nyie mnaacha kuhubiri Injili na mnaanza kuhubiri hoja za Vyama vya Siasa, wanajisikiaje hawa?
Naomba kuwauliza TEC, kwa nini hamkusubiri Tume ya Uchunguzi ifanye kazi kisha ilete majibu? Mnajua tume itakuja na majibu gani? Hivi ikija na majibu ya sababu za msingi za namna vyombo vilivyokabiliana na matukio yale, mtabadilisha andiko na tamko lenu?
Mababa Askofu ina maana hamjui kuwa kinachoendelea ni ushawishi mkubwa wa watu wasioitakia mema Tanzania?
Mababa Askofu hamsikii hoja za kwamba mnaipiga vita Serikali hii kwa sababu Rais sio Mkatoliki? Kwamba mmeshaona Kanisa Katoliki ndio pekee lenye haki ya kuweka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?
Labda niulize Rais Samia amefanya mangapi ambayo huko nyuma Kanisa Katoliki lilinyimwa? Hivi mnadhani Serikali ikikunjua makucha Kanisa litabaki salama? Mmesahau jinsi Hayati Rais Magufuli alivyowashughulikia? Mmesahau jinsi Rais Samia alivyowasaidia? Kwa nini mnafanya mipango ya kumkwamisha huyu Mama Rais Samia. Amekosa nini?
Hayo madai ya wanasiasa ambayo na nyinyi mmefanya ajenda yenu hamjui majibu yake?
Hamjui k**a Rais Samia ameahidi katika kipindi cha miaka mitano tutapata Katiba mpya? Hamjasikia ahadi ya maridhiano? Hamjasikia mipango ya mageuzi ya kiuchumi? Hamna ufahamu na falsafa ya R nne na namna ambavyo Rais Samia ameanza kuzitekeleza?
Mababa Askofu hamjui namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita imechukua hatua madhubuti za kujenga uchumi na kukuza kipato cha Watanzania? Hamjui namna ambavyo Rais Samia ameongeza fursa za ukuaji wa demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kisiasa na uhuru wa masuala mengine mengi? Mmesahau jinsi mambo haya yalivyobanwa wakati wa utawala wa Mkatoliki mwenzetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli?
Naomba kuwasihi, msitukwaze Wakatoliki, msiwagombanishe Watanzania na Serikali yao, msiwe chanzo cha machafuko ya nchi. Nawasihi kwa unyenyekevu, fanyeni jitihada za kuliunganisha Taifa, na k**a haiwezekani basi kaeni kimya muache Wadau wengine waunganishe Taifa.
Mwacheni Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aongoze Tanzania, acheni Tanzania idumishe amani na waacheni Watanzania waamue wanataka nchi iendaje.
Naiomba Serikali isisite kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi wa Kanisa Katoliki ambao wanatupeleka katika mwelekeo huu. Mimi ni Mkatoliki, najua sio viongozi wote wa Kanisa hili wanafurahishwa na mwenendo huu, najua najua ubabe na utamaduni usio wa kidiplomasia ndani ya Kanisa unaficha sauti za Wakatoliki ambao wanatofautiana na msimamo wa NEC. Acheni kufanya hivyo viongozi wangu, mnatukwaza waumini.
Kaeni mbali na siasa na pambaneni na kueneza Injili na kuunganisha watu wa Mungu. Sambazeni upendo na usuluhishi, tangazeni amani na upendo na muwe na furaha pale nchi inapokuwa na amani.
Tumsifu Yesu Kristo.