05/08/2026
Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Ester Amos Bulaya, amesema kuwa msingi wa kupata viongozi bora ni kuwekeza katika elimu, akieleza kuwa kiongozi bora ni yule anayeacha alama ya utendaji na maendeleo yenye manufaa kwa wananchi wake.
Bulaya ametoa kauli hiyo leo, Agosti 5, 2026, wakati akiendelea na ziara yake ndani ya jimbo hilo, ya kukabidhi mashine 10 za kunakili nyaraka (photocopy) kwa shule 10 za msingi na sekondari zilizopo katika kata 10 za Jimbo la Bunda Mjini. Amesema lengo la msaada huo ni kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa wanafunzi pamoja na walimu.
Aidha, Mbunge Bulaya amesema ataendelea kuboresha miundombinu ya huduma za jamii katika jimbo lake, ikiwemo barabara, upatikanaji wa maji safi na salama, pamoja na kuhakikisha wananchi wanaoishi katika mitaa ya pembezoni mwa mji wanaunganishiwa huduma ya umeme kwa gharama ya shilingi 27,000.
Amesema pamoja na Serikali kujenga shule nyingi nchini, bado changamoto kubwa ipo katika ukarabati wa miundombinu ya elimu kutokana na kutotengwa kwa fedha za kutosha kwa ajili ya matengenezo. Amefafanua kuwa bajeti ya Taifa ni takribani shilingi trilioni 3.5, huku Jimbo la Bunda Mjini likihitaji zaidi ya shilingi bilioni 2.4 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya shule.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania Wilaya ya Bunda mwalimu dotto luhende amesema kupatikana kwa mashine hizo za kunakili nyaraka kutarahisisha shughuli za ufundishaji na ujifunzaji, na kwamba anaamini hatua hiyo itachangia kuimarika kwa kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika halmashauri hiyo.
Nao madiwani wa Kata za Guta, Bunda Stoo na Nyasura wamemshukuru Mbunge Ester Bulaya kwa kutatua changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa mashine za kunakili nyaraka, wakisema msaada huo utaboresha utoaji wa huduma za elimu katika shule zilizopo kwenye kata zao.
Hadi kufikia sasa, jumla ya shule sita kutoka kata sita zimepokea mashine hizo za kunakili nyaraka (photocopy). Kata zilizonufaika katika awamu hiyo ni Sazira, Manyamanya, Kabasa, Guta, Bunda Stoo na Nyasura.