12/01/2026
Zaidi ya Watoto 2,500 wa kawaida na wenye mahitaji maalumu katika Jimbo la Kivule wamenufaika na ugawaji wa vifaa mbalimbali vya Shule vyenye thamani ya Tsh. milioni 40 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Mbunge wa Jimbo hilo, Ojambi Massaburi .
Vifaa vilivyogawiwa jana January 11, 2026 ni pamoja na sare za shule, taulo za k**e, sabuni, miswaki na mahitaji mengine ya msingi yanayowasaidia Wanafunzi kuendelea na masomo katika mazingira bora na rafiki.
Akiongea wakati wa zoezi hilo, Mbunge Ojambi Masaburi amesema ugawaji wa vifaa hivyo ni hatua ya kuwasaidia Watoto kutoka Familia zenye kipato cha chini pamoja na kuhakikisha Wanafunzi, wakiwemo wenye mahitaji maalumu, hawakatishwi masomo kutokana na ukosefu wa mahitaji ya msingi.
Amesema kuwa jitihada hizo zinaenda sambamba na maboresho makubwa ya miundombinu ya elimu yanayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo ujenzi wa Shule mpya, madarasa ya kisasa na kuimarishwa kwa upatikanaii wa walimu.
Ugawaji huo umefanyika kupitia Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Kivule kwa kushirikiana na Mtara Wanje Foundation, Apex Foundation pamoja na Mfuko wa Jimbo, kwa lengo la kupunguza changamoto ndogondogo zinazowakabili wanafunzi katika safari yao ya elimu.