07/10/2025
Tukiruhusu Ukatili Utawale Tanzania, Tutawezaje Kuwa na Nchi ya Amani?
Niliwahi kufundisha shule fulani ambapo, mara mojamoja, mwalimu mkuu wake aliamua kwamba, kutokana na utundu au uzembe fulani, wanafunzi wapewe extra drill. Ndiyo.
Sijawahi kuwepo jeshini, lakini walimu wenzangu waliniambia kwamba ni hiyohiyo waliyopitia wengine wakiwa JKT. Lakini baadaye walikiri kwamba baadhi ya adhabu walizotoa zilikuwa zimepigwa marufuku jeshini, hasa kwa wanawake, na hii ilikuwa shule ya wasichana.
Na extra drill sio mchezo. Sikujua. Sasa kwa kuwa walimu wote walitakiwa kushiriki kutoa hiyo extra drill, ikabidi niwemo na mimi. Wanafunzi walikimbizwa, wakaviringishwa kwenye mchanga, na hata kulazimika kulala kwenye mifereji yenye maji baridi sana, wakarushwa hata kichura.
Hadi wanafunzi karibu wote walikuwa wanalia, wengine wanatoa udenda k**a vile wanataka kufa, wanashindwa kusimama, lakini wanapigwa viboko hadi wasimame na kuanguka tena.
Wengine walizimia, wengine walipelekwa zahanati baadaye lakini adhabu iliendelea … iliendelea … iliendelea hadi baada ya masaa, mwalimu mkuu, ambaye ninao uhakika alikuwa anaangalia akiwa nyumbani kwake maana nyumba ilikuwa ndani ya eneo la shule, hadi akatoka.
Dah maigizo!
Alitukimbilia sisi walimu akihema maana hakuwa mwembamba, akiasa: “Jamani walimu, inatosha, inatosha, jamani, maskini wanafunzi inatosha.”
Ni yeye aliyeagiza iwepo extra drill. Ni yeye aliyeangalia ikifanyika. Na sasa anajidai mwenye huruma sana na kuwasihi walimu waache. “Jamani imezidi,” alitwambia. “Sikujua, basi, basi, basi walimu naomba mwache.” Halafu anawageukia wanafunzi, akiwaambia: “Poleni, poleni, nendeni mkapumzike.”
Yaani ionekane walimu ndio washenzi, yeye mtakatifu. Sijui wanafunzi wangapi walitambua hilo, lakini mimi binafsi nilisikia kichefuchefu mbele ya unafiki wa aina hii.
https://thechanzo.com/2025/10/06/tukiruhusu-ukatili-utawale-tanzania-tutawezaje-kuwa-na-nchi-ya-amani/