03/01/2026
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema wananchi wa Venezuela wameondokana na kile alichokitaja kuwa ni udikteta wa Nicolás Maduro, akieleza kuwa hatua hiyo ni chanzo cha faraja kwa watu wa nchi hiyo.
Kupitia ujumbe aliouchapisha katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, Macron alisema Maduro alidhuru heshima ya wananchi wake kwa kunyakua madaraka na kukanyaga haki na uhuru wa msingi wa binadamu.
Rais huyo wa Ufaransa amesisitiza kuwa mchakato wa mpito wa uongozi nchini Venezuela unapaswa kufanyika kwa amani, kwa misingi ya kidemokrasia na kwa kuheshimu matakwa ya wananchi.
Aidha, Macron ameeleza matumaini yake kuwa Rais Edmundo González Urrutia, aliyechaguliwa mwaka 2024, ataweza kusimamia haraka mchakato huo wa mpito kwa lengo la kurejesha utawala wa kidemokrasia nchini humo.
Macron amebainisha kuwa kwa sasa anaendelea kufanya mazungumzo na washirika wa Ufaransa katika ukanda wa Amerika ya Kusini kufuatilia maendeleo ya kisiasa nchini Venezuela.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Ufaransa ipo macho na imejipanga kikamilifu, hasa katika kuhakikisha usalama wa raia wake waliopo nchini Venezuela, kutokana na hali ya sintofahamu inayoendelea.