23/09/2025
Kocha Mkuu wa Yanga SC, Romain Folz, ameeleza furaha yake kwa kuwa na kikosi kipana chenye wachezaji wenye uwezo wa kucheza katika kila mchezo, akisisitiza kuwa kila mmoja ana nafasi ya kuonyesha thamani yake.
Folz amesema kila mchezaji kwenye timu hiyo ni muhimu, na kutokuwepo kwa mchezaji fulani kwenye mechi moja haina maana kwamba hana nafasi katika mipango ya klabu.
“Ni lazima nichague wachezaji 11 wa kuanza, lakini kila mmoja kwenye kikosi chetu ni sehemu ya nguvu ya timu. Kuna siku utaona mchezaji fulani akicheza, na siku nyingine nafasi yake ikachukuliwa na mwingine, yote hayo ni sehemu ya mpango,” alisema.
Akiwaelekea mashabiki kuelekea pambano la ligi kuu dhidi ya Pamba Jiji linalochezwa kesho Jumatano kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Folz alisema wanakwenda dimbani wakiwa na dhamira moja — kuanza msimu kwa ushindi.
“Tunakwenda kucheza mchezo wetu wa tatu wa ushindani. Ni mchezo muhimu sana kwetu na maandalizi yamekuwa mazuri. Tumefanya pre-season yenye tija, ambayo itatusaidia msimu mzima. Malengo yetu ni kila mechi kupata alama tatu, kwa sababu Yanga ni timu kubwa na inalenga kutwaa ubingwa,” aliongeza.
Kocha huyo alisisitiza kwamba msimu huu mashabiki wategemee kuona mabadiliko ya kikosi mechi kwa mechi, kutokana na mpango wa kumpa kila mchezaji nafasi kulingana na bidii yake mazoezini na kwenye michezo.
“Jambo la msingi ni kwamba tuna kikosi imara, wachezaji wenye ari ya kupigania jezi ya Yanga, na kwa pamoja tutaweza kufanikisha malengo ya klabu,” alisema.
Kwa upande wa wachezaji, beki Frank Assink alitoa kauli ya kuwatia moyo mashabiki, akisema: “Wote wanajua Yanga ni timu bora. Kesho tunataka mashabiki waje kuona kiwango kizuri kutoka kwetu.”
NB: USISAHAU KU-SUBSCRIBE CHANNEL YA WATANI WA JADI YOUTUBE
*********************************************