02/09/2026
KATHMANDU, NEPAL : Idadi ya watu waliofariki kutokana na mafuriko makubwa yaliyolikumba taifa la Nepal imeongezeka na kufikia 1,127, huku watu wengine 4,858 wakiwa bado hawajulikani walipo.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi nchini Nepal imeeleza kuwa vikosi vya uokoaji vinaendelea na juhudi za usiku na mchana kusaka majeruhi na kuopoa miili ya waliofariki, ikiwa ni siku ya nane tangu maafa hayo yatokee katika eneo la milima ya Himalaya.
Msemaji wa polisi ametoa mchanganuo wa maeneo yaliyoathirika zaidi ambapo miili 348 imepatikana wilayani Chitwan, 217 kutoka Nawalparasi Mashariki, 190 kutoka Nawalparasi Magharibi, na 155 katika eneo la Nuwakot. Maeneo mengine yaliyokumbwa na maafa hayo ni pamoja na Gorkha ambako miili 66 imeopolewa, Dhading (59), Rasuwa (45), na miili 38 ikipatikana wilayani Tanahu.
Hali ya dharura inaendelea huku mashirika ya kutoa misaada yakihimiza usaidizi wa haraka kwa waathirika.