16/01/2026
Takribani wafuasi saba wa upinzani nchini Uganda wameuawa katika vurugu zilizotokea usiku kucha katika mazingira yanayozua mabishano makubwa ya kisiasa, wakati Rais Yoweri Museveni akiongoza kwa kiwango kikubwa katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais uliofanyika Alhamisi.
Kwa mujibu wa upinzani, wafuasi wao walishambuliwa na vikosi vya usalama walipokuwa wamekusanyika katika makazi ya mbunge wa upinzani Muwanga Kivumbi huko Butambala, takribani kilomita 55 kusini-magharibi mwa mji mkuu Kampala.
Hata hivyo, polisi wamekanusha madai hayo na badala yake kuilaumu upinzani kwa kuchochea vurugu.
Tume ya Uchaguzi ilitangaza Ijumaa mchana kuwa, kwa kuzingatia matokeo kutoka asilimia 60 ya vituo vya kupigia kura, Rais Museveni alikuwa anaongoza kwa asilimia 75 ya kura zote zilizohesabiwa, akifuatiwa na kiongozi wa upinzani Bobi Wine kwa asilimia 21.
Akizungumza na shirika la habari la AFP, Mbunge Muwanga Kivumbi alisema askari na polisi walifyatua gesi ya kutoa machozi na baadaye risasi za moto dhidi ya mamia ya watu waliokuwa wakifuatilia matokeo ya awali katika makazi yake.
Alidai kuwa watu kumi waliuawa ndani ya nyumba yake.
Madai hayo yalithibitishwa na mwanaharakati wa haki za binadamu, Agather Atuhaire, katika mazungumzo na shirika la habari la Reuters.
Hata hivyo, msemaji wa polisi wa eneo hilo, Lydia Tumushabe, amepinga kauli hizo akisisitiza kuwa polisi walilazimika kutumia nguvu kwa kujilinda baada ya kile alichokitaja k**a shambulio la “kundi la wahuni wa chama cha NUP” dhidi ya kituo cha polisi, pamoja na mpango wa kuvamia kituo cha kujumlisha kura.
Alidai kuwa washambuliaji walikuwa wamejihami kwa mapanga, mashoka na vifaa vya kuwasha moto, na kwamba angalau watu saba walipoteza maisha.
Wakati huohuo, waandishi kadhaa wa habari wa ndani wameripoti kuzuiwa na vikosi vya usalama kufika katika makazi ya kiongozi wa upinzani Bobi Wine, yaliyoko eneo la Magere, Kampala.
Chama cha NUP kilidai kupitia mtandao wa X kuwa maafisa wa usalama walivuka uzio wa makazi hayo kinyume cha sheria na kuanza kuweka mahema ndani ya kiwanja chake.
Kwa upande wake, msemaji wa polisi Kituuma Rusoke aliambia kituo cha televisheni cha NBS kuwa Bobi Wine, k**a mgombea wa urais, alikuwa “mtu wa kuzingatiwa,” akiongeza kuwa uwepo mkubwa wa vikosi vya usalama katika eneo la makazi yake ulikuwa ni kwa lengo la kuhakikisha usalama wake binafsi.
Tukio hili limeongeza mvutano wa kisiasa nchini Uganda, huku mashirika ya haki za binadamu na wadau wa demokrasia wakitaka uchunguzi huru na wa haraka kuhusu vifo na matumizi ya nguvu katika kipindi cha uchaguzi.