16/09/2025
Masista wanne Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, na Dereva wao, wamefariki kwa ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Bukumbi, mkoani Mwanza, walipokuwa wakielekea uwanja wa Ndege, baada ya gari yao kugongana uso kwa uso na Lori majira ya saa5 usiku wa jana Septemba 15,2025.
Waliofariki ni, Sr. Lilian Kapongo (55), Mama Mkuu wa Shirika, Sr. Nerina Simeon (60), Katibu Mkuu wa Shirika na raia wa Italia, Sr. Damaris Matheka (51), Mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana Bukumbi, Sr. Stellamaris Muthini (48), mtawa raia wa Kenya, Boniface Msonola (53), Dereva.
Masista hawa walienda jimboni (Kahama) kwa ajili ya Nadhiri za Daima za wenzao watatu, katika adhimisho lililofanyika siku ya Jumamosi. Jana asubuhi walianza safari kutokea Kahama kuelekea Mwanza kabla ya kurudi Dar es Salaam. Majira ya saa 5 usiku, wakiwa wanatokea kwenye Jumuiya yao Bukumbi - Mwanza kuelekea Uwanja wa Ndege, wakapata ajali na kufariki dunia.
Mtu pekee aliyenusurika na mauti katika ajali hiyo ni Sr. Pauline Mipata (20), Matron wa shule ya wasichana Bukumbi, ambaye hata hivyo amejeruhiwa vibaya na kwa sasa yupo chumba cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Bugando.