29/08/2026
JENGENI TASWIRA NJEMA YA JESHI LA UHIFADHI KWA WANANCHI — WAZIRI KIJAJI
MLELE, KATAVI — Agosti 29, 2026:
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Dkt. Kijaji (PhD) amewataka askari na maafisa wa uhifadhi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, huku wakiepuka matumizi ya nguvu yasiyo ya lazima, ili kujenga na kuimarisha taswira njema ya Jeshi la Uhifadhi mbele ya wananchi.
Waziri Kijaji ametoa maelekezo hayo leo, Agosti 29, 2026, wakati akifunga rasmi mafunzo ya awali ya kijeshi kwa askari wapya 328 waliohitimu mafunzo katika Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi Mlele.
Amewataka askari hao kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo, uadilifu, weledi na uwajibikaji, wakizingatia viapo vyao na kutotetereka katika kutekeleza wajibu wao licha ya changamoto wanazoweza kukutana nazo katika maeneo ya kazi.
Aidha, Waziri Kijaji amewakumbusha askari hao kujiepusha na vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji wa maadili ya utumishi, akisisitiza kuwa Serikali haitamvumilia mtumishi yeyote atakayejihusisha na vitendo hivyo.
Amesema nidhamu, uadilifu na heshima kwa wananchi ni misingi muhimu katika kujenga imani ya jamii kwa Jeshi la Uhifadhi na kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia haki.
WANANCHI WAHUSISHWE KATIKA UHIFADHI
Katika hatua nyingine, Waziri Kijaji amewaelekeza Wakuu wa Taasisi na Makamishna wa Uhifadhi kuhakikisha kuwa Wimbo wa Uhifadhi unafundishwa katika shule, hatua inayolenga kuwajengea wanafunzi uelewa wa umuhimu wa uhifadhi, uzalendo na uwajibikaji kwa mazingira tangu wakiwa katika hatua za awali za elimu.
Amesema ushiriki wa wananchi ni msingi muhimu wa mafanikio ya uhifadhi endelevu, hivyo ni muhimu kuanza kujenga utamaduni wa uhifadhi na uzalendo kuanzia kwa kizazi cha vijana.
Waziri Kijaji amesisitiza kuwa Jeshi la Uhifadhi linapaswa kuwa sehemu ya jamii na kufanya kazi kwa kushirikiana na wananchi, huku likilinda rasilimali za Taifa kwa weledi, nidhamu na kuzingatia sheria.
“Uhifadhi una nguvu zaidi pale wananchi wanapokuwa sehemu ya uhifadhi.”