22/07/2025
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (Mwana FA), leo amekutana na kufanya kikao maalum cha usuluhishi kati ya msanii wa muziki wa kizazi kipya, Billnass, na msambazaji wa kazi za muziki, Mx Carter.
Kikao hicho kimefanyika kufuatia malalamiko ya hadharani yaliyotolewa na Billnass kupitia mitandao ya kijamii, ambapo alieleza kutoridhishwa na namna kazi zake zinavyosambazwa na kutopata faida inayostahili kupitia majukwaa ya kidigitali.
Malalamiko hayo yamezua mjadala mpana kuhusu maslahi ya wasanii na usimamizi wa haki zao za kazi za sanaa.
Katika kikao hicho, Naibu Waziri amesikiliza pande zote mbili na kutoa mwongozo wa kisheria na kiutawala kwa lengo la kuhakikisha haki na maslahi ya msanii yanalindwa bila kuvunja mikataba iliyopo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wasanii na wasambazaji, pamoja na kuhimiza matumizi ya mifumo rasmi ya usambazaji inayohakikisha uwazi wa mapato.
“Kama Wizara, tutaendelea kuwa sehemu ya kutafuta suluhu kwa changamoto za wasanii wetu, lakini pia ni jukumu la pande zote kuhakikisha mikataba inazingatia haki na uwiano wa mapato,” alisema Mhe. Mwinjuma.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na maafisa kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), pamoja na COSOTA, ili kuhakikisha suluhu ya kudumu inapatikana kwa misingi ya haki na uwazi.
Hii ni hatua muhimu katika kulinda hadhi ya msanii wa Kitanzania na kuimarisha tasnia ya muziki nchini.