02/04/2024
Simba ina nafasi, Yanga inaweza
Na Mwandishi WETU
MAMBO sasa yamebadilika na “meza ya historia imepinduliwa” baada ya timu za soka za Tanzania kuweza “kuwavimbia” na hata kuwafunga Waarabu.
Timu kutoka Misri, Tunisia, Algeria na Morocco, zilikuwa na uhakika wa kuzifunga timu za Tanzania na hazikuwa na hofu yoyote; iwe ndani ya nchi zao au zinazpokuwa Dar es Salaam.
Miongo k**a miwili iliyopita timu kutoka nchi hizo za Kiarabu, ambayo ilipangwa kucheza na timu yoyote ya Tanzania, ingeweza kufika Dar es Salaam asubuhi ya siku ya mechi, jioni ikacheza na usiku huohuo ikaondoka kurudi kwao, huku ikiwa imepata ushindi mkubwa.
Hata hivyo, mambo yamekuwa tofauti sana na sasa Waarabu wanacheza na timu za Tanzania, wanakuwa na adabu.
Ipo mifano mingi, lakini moja ni mechi ya kwanza na robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwishoni mwa wiki iliyopita – Machi 29, timu bora Afrika wakati huu, Al Ahly ya Misri, ililazimika kuja na karibu kila kitu wanachokihitaji kwa ajili ya maandalizi ya mechi yake dhidi ya Simba.
Tena walikuja siku kadhaa kabla ya siku ya mechi. Lakini Al Ahly, ambayo inahesabika kuwa ni timu bora Afrika, iliambulia ushindi mwembamba wa goli moja tu na huo ukiwa ni ushindi wa kwanza wa timu hiyo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa katika miaka ya hivi karibuni.
Takriban miaka mitano, Al Ahly walikuwa hawajawahi kupata ushindi katika uwanja huo.
Wakati huohuo, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini nayo imekiona cha moto juzi – Jumamosi, Machi 30, baada ya kutumia maarifa yao yote, lakini wakaambulia suluhu wakicheza na Yanga katika mchezo mwingine wa robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika.
Kabla ya mchezo huo, watu wengi waliaminishwa, kupitia uchambuzi uliojikita katika rekodi za timu hiyo katika miaka ya hivi karibuni, kuwa itapata ushindi mbele ya Yanga. Lakini hali haikuwa hivyo.
Orodha ya wachezaji wa mechi hiyo ilipotolewa, Yanga ikiwa haina wachezaji wake muhimu kadhaa, wengi wakaamini kuwa kipigo kwa Yanga hakiepukiki.
Lakini Yanga ilifanikiwa kuibana Mamelodo na kutoka nayo suluhu na kuwaacha watu wengi na mshangao.
Mechi hizi mbili za robo fainali ya Klabu Bingwa Barani Afrika zimetuacha funzo kubwa.
Kuwa mechi mbili za robo fainali zimechezwa Dar es Salaam zikihusisha timu za Tanzania na hii inamaanisha kuwa Tanzania imeingiza timu mbili katika hatua hiyo kubwa ya mashindano makubwa Afrika.
Katika nchi zote zilizoshiriki mashindano hayo tangu awali hakuna nchi yoyote ambayo imefanikiwa kuingiza timu mbili katika hatua hiyo isipokuwa Tanzania.
Na matokeo ya mechi za kwanza yanaonesha kuwa Simba na Yanga hazikufika katika hatua hiyo kwa kubahatisha.
Hali hii inaweza isishangaze sana kwa Simba ambayo katika kipindi kifupi imefanikiwa kufika mara tano katika mashindano ya Afrika, ikifanya hivyo mara nne katika mashindano ya Klabu Bingwa na mara moja katika Kombe la Shirikisho.
Yanga ilianza kuonesha mabadiliko mwaka jana ambapo ilifanikiwa kufika katika fainali za Kombe la Shirikisho kwa kutolewa kwa kanuni ya goli la ugenini.
Historia inaonesha kuwa katika miaka ya hivi karibuni, Simba imeingia robo fainali ya mashindano ya Afrika mara tano na mwaka jana Yanga ilifika fainali.
Ingawa historia haichezi mpira, lakini ni muhimu kukubali kuwa historia inajengwa na uhalisia. Hivyo, uhalisia ni kuwa viwango vya kucheza vya Simba na Yanga vimeimarika katika miaka ya hivi karibuni.
Hivyo, ingawa baadhi ya watu wameshaikatia tamaa Simba baada ya kufungwa goli moja Dar es Salaam, lakini uhalisia unaonesha kuwa timu hiyo bado ina nafasi ya kuitoa Al Ahly na kusonga mbele katika mashindanipo hayo.
Aidha, suluhu iliyoipata Yanga mbele ya Mamelodi huku ikipungukiwa na wachezaji wake muhimu, inadhihirisha kuwa timu hiyo inaweza kuitoa Mamelodi katika mechi ya marudiano itakayofanyika Aprili 5 huko Afrika Kusini.
Viwango
Lakini kwa ujumla ukiangalia timu zilizoingia kwenye hatua ya robo fainali ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika msimu huu, utabaini kuwa hali ya mchezo wa soka katika eneo la Afrika Mashariki na Kusini imeboreka kwa kiasi kikubwa.
Kati ya timu nane zilizoingia katika hatua hiyo, tano zinatoka katika ukanda wa SADC. Timu hizo ni Yanga na Simba kutoka Tanzania, Mamelod ya Afrika Kusini, TP Mazembe ya DRC na Atletco de Angola kutoka Angola.
Kuna timu moja tu kutoka Afrika Magharibi na Afrika Kaskazini imetoa timu mbili.
Miaka kadhaa iliyopita hakuna mtu alitarajia hali k**a hiyo. Ukiacha TP Mazembe, hakuna timu nyingine iliyokuwa inajitutumua kufika hatua hiyo kutoka eneo la SADC mpaka pale Mamelodi nayo ilipojiingiza kwa kasi kwenye soka la Afrika. Sasa hivi Simba na Yanga nazo zimeingia huko.
Hii inaonesha kuwa ule utawala wa soka kwa nchi za kaskazini na magharibi mwa Afrika, sasa mzani umegeuka.