25/08/2025
Tanzania imeanza ujenzi wa maabara kubwa na ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini, ambayo itakuwa kubwa kuliko zote katika nchi za Afrika Mashariki na Kati. Maabara hii itatoa huduma za kimaabara kwa ubora wa hali ya juu na kwa haraka kwa wadau wa sekta ya madini nchini.
Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde, wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa maabara hiyo katika eneo la Kizota, Jijini Dodoma.
“Tunamshukuru Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa mageuzi makubwa katika sekta ya madini na kwa kuandika historia ya ujenzi wa maabara hii ya kisasa, miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) mwaka 1925.
Leo tunaandika historia kwa kuanza ujenzi wa maabara kubwa itakayokuwa na mitambo na vifaa vya kisasa vinavyotoa huduma za kimaabara ndani na nje ya nchi. Hii itakuwa ni ukombozi mkubwa kwa wadau wa sekta ya madini kupata taarifa sahihi za kimaabara kwa wakati na zenye ubora wa hali ya juu. Ni imani yangu maabara hii itachochea ukuaji na maendeleo ya sekta ya madini,” alisema Mavunde.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST), Dkt. Notka Huruma Batenze, amesema maabara hii ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini italeta tija kubwa kwa wadau wa sekta ya madini na kurahisisha upatikanaji wa huduma hii muhimu kwa maendeleo ya sekta ya madini.
Gharama za ujenzi wa maabara hii zinakadiriwa kufikia shilingi bilioni 14.3, huku muda wa kukamilisha ujenzi ukikadiria kuwa siku 690.