25/09/2026
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungia msanii Godfrey Tumaini maarufu k**a Dudubaya kujihusisha na shughuli za sanaa kwa namna yoyote ile, na kumtoza faini ya Shilingi Milioni Tatu.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na BASATA, uamuzi huo umetokana na tukio lililotokea Septemba 19, 2026 katika Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Flava lililofanyika katika Viwanja vya General Tyre, jijini Arusha.
BASATA imesema wakati akitumbuza, Dudubaya hakuizingatia Mwongozo wa Maadili katika kazi za sanaa, na alitenda kosa ambalo linavunja heshima ya msikilizaji au mtazamaji, kinyume na Kanuni ya 20(a) ya Kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa, Tangazo la Serikali Na. 137 la tarehe 22 Mei 2026.
Baraza limesema baada ya kufanya tathmini na utekelezaji, limejiridhisha kuwa msanii huyo alitenda kosa hilo kwa makusudi, na imebainika kuwa ana desturi ya kukosea taratibu zinazosimamia uendeshaji wa matamasha ya sanaa nchini kwa makosa yanayojirudiarudia.
Wakati huo huo, BASATA pia imemchukulia hatua Mratibu Mkuu wa Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Flava kwa kushindwa kusimamia matamasha kwa mujibu wa Sheria.
Mratibu huyo pia ametoza faini ya Shilingi Milioni Tatu na kufungiwa kujihusisha na shughuli za sanaa hadi atakapotekeleza maamuzi hayo.
BASATA imetoa rai kwa wasanii na wadau wa sanaa kuhakikisha wanazingatia Sheria, Kanuni, Miongozo na Maadili ya Mtanzania wanapotekeleza kazi zao za sanaa.