25/08/2026
Balozi Nchimbi Atangaza Kujiuzulu, Makamu wa Rais
Agosti 25, 2026— Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo, akisema amefanya uamuzi huo kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika taarifa yake yenye kichwa “Taarifa kwa Umma" iliyotolewa leo Agosti 25, 2026, Balozi Nchimbi amesema ameamua kujiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais kwa kuzingatia *Ibara ya 50(2)(c) ikisomwa kwa pamoja na Ibara ya 149(2) ya Katiba*, kuanzia *tarehe 4 Septemba 2026*.
Balozi Nchimbi amesema uamuzi huo unafuatia ahadi aliyompa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo tarehe *27 Agosti 2025* alimwahidi kuwa angemsaidia yeye na nchi kwa uwezo na uaminifu wake wote.
> “Pia, nilimwahakikishia kuwa siku yoyote akiona anahitaji Makamu mwingine wa Rais, nitaachia nafasi hii,” amesema Balozi Nchimbi katika taarifa hiyo.
Amesema amejiridhisha kuwa Rais Samia anatarajia mabadiliko, hivyo ameamua *kutimiza ahadi yake* kwa kuachia nafasi hiyo.
Katika taarifa hiyo, Balozi Nchimbi pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa imani waliyonayo kwake.
“Natumia nafasi hii pia kuwashukuru Watanzania wote kwa ushirikiano mkubwa mlionipa wakati wote nilikuwa katika utumishi wa umma,” amesema.
Aidha, amewaahidi Watanzania kuwa ataendelea kuwa **raia mwema wa Tanzania**, akisisitiza dhamira yake ya kuendelea kulitumikia taifa kwa namna nyingine.
Balozi Nchimbi amekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu Novemba 2025, baada ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Rais Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.