21/09/2026
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umekusanya Sh150.04 bilioni kutokana na tozo za matumizi ya Daraja la Nyerere Kigamboni katika kipindi cha miaka 10 tangu lilipoanza kutumika Mei 2016.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema hayo leo Jumatatu, Septemba 21, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi kati ya menejimenti ya mfuko huo, wahariri na waandishi wa habari chini ya uratibu wa ofisi ya Msajili wa Hazina.
Amesema mradi huo katika ujenzi uligharimu Sh345.20 bilioni, zikiwemo Sh328.74 bilioni za ujenzi na Sh16.46 bilioni zilizotumika kulipa fidia kwa wananchi waliohamishwa kupisha ujenzi wa mradi huo.
“Mradi huo ulipangwa kurejesha fedha zilizowekezwa ndani ya kipindi cha miaka 30 na Juni 2026, NSSF ilikuwa imekusanya Sh150.04 bilioni kutokana na tozo za matumizi ya daraja,” amesema.
Katika kipindi hicho, amesema NSSF pia imetumia Sh25.81 bilioni kwa gharama za uendeshaji na matengenezo ya daraja hilo huku mapato yaliyokusanywa yakiendelea kuchangia katika kurejesha fedha zilizowekezwa kwenye mradi.