13/01/2026
Wadau wa elimu waliosoma katika Shule ya Msingi Monuna, iliyopo Kata ya Nyambureti, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wametoa msaada wa madaftari, kalamu na mabegi kwa wanafunzi wanaotarajiwa kuanza masomo ya sekondari mwaka huu.
Msaada huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya jitihada za wadau hao kuhakikisha wanafunzi wanapata haki yao ya msingi ya elimu katika mazingira bora na yenye usawa, bila kujali changamoto za kiuchumi zinazowakabili.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mwenyekiti wa umoja huo, Joram Agary, alisema msaada huo unalenga kuwapa hamasa wanafunzi hao na kuwasaidia kuanza safari ya elimu ya sekondari wakiwa na vifaa muhimu vya masomo.
“Msaada huu utawasaidia wanafunzi wetu kupata haki ya elimu k**a wenzao na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa usawa,” alisema Agary.
Alifafanua kuwa wazo la kutoa msaada huo lilianzishwa kupitia kundi la WhatsApp la wadau hao, ambapo wanachama walikubaliana kuchangia kwa pamoja na hatimaye kufanikisha zoezi hilo kwa vitendo.
Katika zoezi hilo, jumla ya wanafunzi 14 wamenufaika, ambapo kila mwanafunzi amepatiwa madaftari tisa kwa ajili ya masomo yao ya sekondari, pamoja na kalamu na mabegi.
Wageni na wanachama wengine waliohudhuria tukio hilo ni pamoja na Josinta Garigo, Sayi Marugu, Maritha Mathayo, Mwajuma Mwita, Juma Kitenge na wengineo.
Baadhi ya walimu wa Shule ya Msingi Monuna wakiongozwa na Mwalimu Mkuu Lukas Kosianga, walitoa pongezi kwa wadau hao kwa juhudi walizozionesha, wakisema ni mfano bora wa ushiriki wa jamii katika maendeleo ya elimu.
Walimu wengine waliokuwepo ni pamoja na Paulo Chacha, Baraka Panyako, Theopista Ngoyani na Joseph Mwashi, ambao kwa pamoja waliwataka wadau wengine wa elimu kuiga mfano huo na kuungana katika kutekeleza ajenda ya elimu kwa vitendo kijijini hapo.
Wadau hao wamesema wataendelea kushirikiana na jamii na uongozi wa shule ili kuhakikisha wanafunzi wanapata msaada unaohitajika kwa maendeleo endelevu ya elimu katika eneo hilo.