28/11/2025
SERIKALI YAANZA KUREJESHA MABASI YA MWENDOKASI UBUNGO,KIVUKONI NA GEREZANI
WAKALA wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es salaam (DART) imerejesha huduma za usafiri wa umma katika awamu ya kwanza, kuanzia Ubungo Terminal kuelekea Gerezani, Kivukoni na Muhimbili.
Huduma hiyo imerejea rasmi leo Novemba 28,2025 katika maeneo tajwa ikiwa ni hatua ya mwanzo ya kurejea kwa huduma baada ya uharibifu mkubwa wa miundombinu uliofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa DART, William Gatambi ameeleza hayo akitoa ufafanuzi wa kuanza kurejea kwa huduma hizo baada ya tathmini iliyofanyika ili kubaini maeneo salama kwa ajili ya kurejesha huduma.
Gatambi amesema, wamefanya hivyo wakati ukarabati katika vituo vilivyoathiriwa ukiendelea kwa awamu ili kuhakikisha mfumo mzima unarejea kikamilifu, huku akikiri kuwa kusitishwa kwa huduma kuliathiri sana wananchi, huku wengi wakilazimika kuhangaika kupata usafiri wa uhakika.