
19/08/2022
RIWAYA: NGOME YA GIZA.
MTUNZI: AHMED R. JIRIWA.
SIMU: 0769 805251
0774 122007
SEHEMU YA 03
JIKUMBUSHE ILIPOISHIA.
Huweza kukuua huku unakunywa nao sharubati au unavuta nao sigara, huweza kukuua huku unafanya nao ngono lakini pia unaweza kujikuta unakufa kwa maumivu makali hasa pale wanapoagizwa kutokuua kirafiki. Watu wote hao huishi k**a wafungwa ndani ya gereza hilo na watu hao ni watano tu wanajiita 'Gwala killers.' Serikali inawajua na inajua kuwa wanatumiwa na watu fulani."
"Wameshindwa kuwadhibiti?"
SONGA NAYO....
Alihoji Roi baada ya kuvutiwa na hiyo simulizi. Bwana Mohamed Aziz alimtazama Roi kisha akamwambia.
"Umeshindwa kuvumilia kutulia hadi nimalize?"
"Kwani hizi ni ngano za paukwa pakawa? K**a si hivyo ninayo haki ya kuhoji na ninapohoji natarajia jibu si swali tena k**a ulivyofanya sasa." Aliongea Roi. Bwana Mohamed Aziz akanyanyua chupa ya pombe akaigida kwa funda kadhaa kisha akairejesha mezani. Aliimeza kwanza kabla hata hajaokota kipande cha nyama na kutafuna.
"Unadhani yupo wa kuwazuia Gwala killers, sheria wako nayo wao na nahisi hata bunge la nchi hii linapotunga sheria huwenda ipo sheria hawaiweki wazi yenye lengo la kuwalinda hawa jamaa. Hawazuiliki. Kuna maslahi baina ya watu fulani serikalini na huyu mmiliki wa hili kundi la Gwala killers. Ni mtu mkubwa na maarufu asiyejulikana..."
"Mtu mkubwa na maarufu asiyejulikana?" Alihoji Roi akiikata kauli ya bwana Aziz bila kujali tena.
"Ndiyo, umaarufu wake unaonekana kwa vijana wengi wa hapa mjini. Kuna vijana wanaishi maisha ya kifahari kwa ajili ya mtu huyo, kuna vijana wanaishi kwa kumtegemea mtu huyo pia. Kivipi... Wapo vijana wengi na wafanyabiashara wakubwa hata wasanii mbalimbali, waliobobea kwenye utumivu wa dawa za kulevya wanamuona huyu k**a Mungu wao ingawa hawajawahi kuijua hata sura yake. Unadhani atashindwa kuwa maarufu. Ni maarufu asiyejulikana. Jina lake halijulikani hadi sasa lakini bado yupo, tunaishi nae na anafanya mambo ya kuogopesha. Hata serikali inamtumia mtu huyu." Alijibu bwana Mohammed Azizi.
"Serikali inamtumia kivipi?" Roi alihoji.
"Wanapotaka kuua mtu fulani labda kwa sababu za kisiasa ama vyovyote kwa lengo la kumfunga mdomo, humtumia huyu mtu kuwaagiza vijana wake kutekeleza hilo suala na hujulikana kwa jina la watu wasiojulikana."
"Nimekuelewa vizuri sasa. Nini lengo lako la kutaka niijue simulizi hii?" Roi aliuliza baada ya kuwa ameelewa vizuri.
"Kuna roho mbili hazina hatia nataka ziwe huru Roi."
"Mbona unataka kuniingiza kwenye jambo nisilolitaka na wewe unalijua hilo. Nikifanya hivyo nitakuwa kinyume na endapo nitak**atwa na kutiwa nguvuni jua fika nitahukumiwa k**a haini, mtu afanyae ujasusi kwenye taifa jingine. Adhabu yake ni kifo Aziz, wewe unajua. Unataka nife. Siwezi." Alisema Roi huku akipiga funda la mwisho kwenye chupa ambayo haikuwa na kinywaji kingi. Aliirejesha chupa mezani ikiwa tupu.
"Watu hawa watakufa Roi k**a hawatapata msaada. Nimejaribu kuwatumia watu wengi kwa kuwaambia hili lakini wamejificha mbali kabisa hawataki hata kuniona. Wengine ni wapelelezi mahiri" Alisema Aziz.
"Wamefanya hivyo kwa kuwa wanajua hicho ni kifo. Sasa mimi nitakuwa mpumbavu nikajiue mwenyewe? Siwezi na naomba tuondoke hapa k**a wewe ba..." Alitaka kumalizia kuongea Roi lakini domo lake lilijaa gundi ghafla mara baada ya msichana mrembo aliyepita mbele yao. Alikuwa mrembo haswa kiasi alijikuta akinyanyuka na kutaka kumfuata. Mtoto wa k**e mrefu kwenda juu, mwenye rangi yake nyeupe mwenye nywele alizozisuka rasta tatu na kuziunganisha pamoja nyuma akitengeneza mkia mnene k**a wa mamba au kenge. Alitembea kwa mwendo wa kilimbwende huku akizitikisa nyama zake laini za nyuma k**a hataki. Roi alipiga hatua ya kwanza pili na tatu huku macho yake yakitazamana na yule msichana aliyemuangalia kwa kitambo kifupi kabla ya kutazama mbele. Alijua kuwa amemkosha huyo kijana kwani hata tabasamu lake lilikuwa likimchokonoa Roi kwa makusudi kabisa. Bwana Mohamed Aziz alibakia akimtazama Roi aliyekatisha mazungumzo kwa ajili ya mrembo yule.
"Bado kuna nguvu za ile mitambo iliyomfanya kuwa mashine ya ngono inaendelea kumtafuna huyu kijana, siyo kwa kupenda penda huku!" Alistaajabu bwana Aziz huku akiikumbuka historia ya Roi kule ilikotokea hadi kuwa jasusi maarufu na mahiri.
Roi hakufanikiwa kupiga hatua ya nne kwani alitokea kijana mmoja aliyekuwa akifanya malipo kaunta akamshika kiuno yule mrembo na kuondoka naye taratibu. Roi akabaki ameganda mithili ya mtu aliyeambiwa kuna mtu alikuwa akimchora kwa ajili ya kutengenezwa k**a sanamu la kumbukumbu hapo nchini Ungamo. Macho yakimtoka k**a mwanga wa kurunzi ya kichina. Yule mrembo kabla hajaufikia mlango aligeuka kisha akamfinyia jicho moja Roi akatoka. Bwana Mohamed Aziz alimshika mkono Roi na kumrejesha kitini. Hakujua k**a alisimama kwa lengo la kutaka kuondoka ama kwa lengo lipi, hilo hakulijua alijikuta tu akikaa tena kitini k**a mwehu tu. Tabia hii ya kupenda warembo wala haikumkatisha tamaa Mohamed Aziz kwani aliijua tabia ya mtu huyo na utendaji wake wa kazi ulivyo. Walitulia kwa kitambo kifupi kabla ya bwana Aziz kuyarejesha tena mazungumzo mezani.
"Kuna mzee mmoja anaitwa Mr. Wasika Jerome. Huyu ni mtu wa zamani ni mhandisi na msanifu mbobevu wa majengo ya kale aliyehusika kuchora ramani ya gereza la KIMKI pamoja na kulijenga akishirikiana na wajenzi wengine wabobevu wa nyakati zake. Yeye ndiye mwenye kila kitu kuhusiana na gereza lile. Sijui k**a unanielewa ninapozungumza hivi? Sikia, namaanisha kwamba huyu bwana analijua gereza la KIMKI k**a kahaba anavyozijua kona za vyumba kwenye nyumba za kulala wageni na mahoteli. Huyu mzee wamemk**ata yapata miaka mitano sasa yupo gerezani. Walimchukua kirafiki lengo lao likiwa ni kutaka kuwaonesha njia za siri za gereza lile ili iwe rahisi kwa hawa Gwala killers kutoka kwenda kufanya walichoagizwa kisha kurudi gerezani pasipo kugundulika k**a wanatokea ndani ya gereza hilo. Inaweza kukuchanganya hii. Ukajiuliza kwanini wawe na hofu wakati wamejivika mamlaka. Ingawa gereza la KIMKI halina ulinzi wa kuwazuia wasifanye wanachokitaka lakini wanataka kujilinda ili k**a litatokea jambo la kuwachunguza wasipatikane na hatia yoyote ile. Hivi ndivyo ilivyo. Aliwafanikishia lakini wamemzika huko huko ingawa anaishi vizuri na kula vizuri lakini gereza ni gereza Roi mtu huyu anahitaji uhuru. Hana kosa. Taaluma yake ndiyo inayomteketeza gerezani na serikali yake iliyoshindwa kujitengenezea ukuta mnene wa kushindwa kuingilika kipumbavu na kuchezewa na watu wachache k**a hawa wanaojiita wenye mamlaka. Yeye mwenyewe Wasika alidhani labda wangemwachia baada ya kumshinikiza sana na kuiathiri familia yake. Kumbe wao hawana nia hiyo mawazo yao huwatuma wakidhani huwenda siri zao zingejulikana au zitajulikana wakimwachia hivyo wameamua kumfanya mfugwa huru hadi pale hitimisho la maisha yake watakapoliamua wenyewe au Mungu." Alisema Aziz kwa maelezo marefu kabisa akiwa anamtazama Roi usoni ambaye hakuwa na muda hata wa kumsikiliza tena bwana huyo.
"Twende tuondoke hapa, siwezi kujiingiza huko mimi." Alisema Roi. Bwana Aziz akashusha pumzi nzito baada ya kuona kumbe yote aliyoongea ni bure kwa kijana huyo. Hata hivyo hakukata tamaa akasema.
"Kuna mpelelezi mahiri na mweledi. Yeye alikuwa akikipeleza kifo cha mfanyabiashara mkubwa ambaye alitekwa na kupotea zaidi ya wiki mbili kabla ya maiti yake kukutwa kwenye jaa kubwa la jiji hili ukiwa ndani ya kiroba cha salfeti, ndipo idara yake ikamtuma akipeleleze kifo hicho ili ajulikane aliyetenda unyama huo. Ni siku tatu tu zilitosha kumpoteza kijana huyo na asionekane machoni mwa watu. Sasa ni miaka mitatu kijana huyo hajaonekana. Hakuna mpelelezi aliyekubali kujiingiza kwenye kasumba hiyo. Hata idara yake ya usalama imekuwa kimya sana haizungumzii chochote kuhusiana na jambo hilo. Kijana huyo anajulikana kwa majina Frank Matiale."
"Nani?" Roi aliuliza akiwa na mshangao mkubwa. Ni k**a masikio yake hayakuwa yamesikia vizuri. Bwana Aziz akarejea kulitaja jina hilo na kumueleza kinaganaga kuwa alizipata taarifa za kupotea kijana huyo lakini pia alipata taarifa kuwa kijana huyo anateseka sana ndani ya gereza la KIMKI. Lengo kuu la mateso hayo ni kumfanya akubali kuisaliti serikali, aungane nao ili awe miongoni mwa wauaji wa Gwala killers. Inaaminika Frank hayupo tayari kujiunga na hilo kundi na yupo tayari kufa kuliko kuwa kinyume na kazi yake. Nao wanamfanyia kusudi hawamwachii na wanamwonesha kwamba wana nguvu kuliko hiyo serikali anayoiaminia. Ni aibu kusema maneno haya Roi mbele yako lakini hakuna njia. Hakuna watu wanaweza kujiingiza kwa makusudi gerezani na kusema tunamtaka kijana wetu au tunawataka watu wetu. Wanajitapa kwa kila hali. Anateseka sana Frank kiasi kwamba huwezi kumtazama mara mbili. Wanasema hivyo wakiwa kwenye majumba ya starehe. Inasemekana wamepanga kumtesa hadi kifo chake k**a ataendelea kusimamia msimamo wake. Hakuna jeshi, polisi wala nini wote kimya hadi hata mimi naogopa kuzungumza." Roi alijikuta mwili ukimsisimka, damu zilikuwa zikimchemka si haba baada ya kumkumbuka rafiki yake aliyemsaidia kwenye ile misheni ya kuikomboa Ungamo kwa watu madhalimu waliotaka kuiangamiza Ungamo na Tanzania. Alimkumbuka maana kwenye misheni hiyo Frank alijiita Frank kichaa na kweli alikuwa kichaa.
Kweli Roi alifika nchini hapo kwa ajili ya kuifaidi likizo yake aliyopewa na kitengo chake baada ya kuimaliza shughuli ngumu iliyotaka kuondoka na maisha yake huko nchini Uganda. Lakini si kwa Frank lazima ajiingize mzimamzima tena anajiingiza bila hata kitengo chake kujua. Hakujua k**a alikuwa akitaka kujipeleka mwenyewe kwenye shimo la mauti.
Hakujua.
Baada ya kuwa amejipa utayari wa kuingia kwenye hiyo kazi na ni kwa lengo moja tu la kumkomboa rafiki yake, alianza kumuuliza maswali bwana Aziz kuwa yeye habari zote hizo alikuwa akiambiwa na nani maana amekuwa akizijua siri nyingi za hao Gwala killers. Bwana Aziz akasema kuwa mbali na wao wenyewe G Killers kujitapa ovyo wakiwa kwenye majumba yao ya starehe, pia kuna askari jela mmoja ambaye anafanya kazi kwenye gereza hilo ndiye anayemfikishia hizo habari.
"Kabla sijaachana na masuala ya jeshi na kupewa kazi ya siri na mkuu wa nchi, nilijenga ukaribu mkubwa sana na askari jela huyo kwa kuwa nilifahamu anafanya kazi wapi na nilifanya hivyo ili kupata habari za gereza lile kabla hata huu uvundo haujaanza kunuka na kuchafua hali ya hewa ya taifa. Nilimfahamu kwa roho yake mbaya maana yeye na wenzake ndiwo tuliokuwa tukiwatumia kutesa watu wetu watukutu walioshindikana katika sehemu mbalimbali za shughuli zetu wakati huo gereza lile likitumika kisheria baada ya kupinduliwa sheria chafu zilizowahi kuwekwa na Rais wa awamu ya pili wa nchi hii aliyekuwa ametunga sheria za kujilinda yeye mwenyewe ili aishi miaka mingi madarakani. Hivyo akalitumia lile gereza kuwaangamiza wanasiasa wote waliokuwa wakimpinga. Watuhumiwa tunapowafikisha kwenye gereza hilo maarufu kwa kunyoosha watuhumiwa sugu basi huyo askari ndiye anayeongoza jopo la watesaji. Tulijenga ukaribu mkubwa sana hata nilipokuja kustaafu bado nilikuwa karibu na huyu ingawa nilijua kwa kipindi hiki anatumiwa vibaya na wale watu washenzi ila yeye hajui k**a mimi najua. Umri wake ni mkubwa lakini bado analitumikia lile gereza kwa kuwa ni mtesaji mmoja hatari sana aliyeishi akitesa kwa miaka mingi na hakuna siri inayofichwa k**a umesogezwa mbele ya mtu huyo." Ndivyo ambavyo alijibu Bwana Mohamed Aziz pindi alipoulizwa.
"Anaitwa nani huyo mtu na anaishi wapi hapa mjini?" Aliuliza Roi.
"Anaitwa Matole Gimba ila kwa jina lake maarufu la utani kutokana na matendo yake wanamuita Jeki simba. Anaishi huko mjini Sami ado kwenye mji uliojitenga unaotwa Majito, ndiko liliko jumba lake la kifahari. Liko juu ya mwamba mmoja mkubwa sana. Amepata pesa nyingi kwa kazi yake ya utesaji ukiachilia mbali mshahara wake anaoupokea kwa kila mwisho wa mwezi. Ukimtazama humdhanii k**a ni mtu mwenye roho mbaya ya kuogopwa. Ni rahisi kukukutanisha naye ni mtu wangu wa karibu sana." Alijibu bwana Aziz.
"Umesema anaishi kitajiri na anapata pesa nyingi kwa shughuli zake za utesaji?"
"Ndiyo,"
"Sitaki unikutanishe naye najua hawezi kuwa rafiki mwema kwangu huku akijua anakwenda kukitia dosari kibarua chake. Inatosha kwa kunielekeza anapokaa. Najua nitampata nikimtaka. Unakutana naye vipi hapa mjini?"
"Pamoja na utu uzima alionao lakini hajabahatika kuoa. Amebahatika tu kuzaa na kahaba hivyo ana mtoto mmoja wa kiume ambaye yupo nchini Afrika ya kusini. Anaishi huko. Anapenda sana anasa hasa mabinti wadogo waliyokosa maadili na kwenda kuiuza miili yao kwenye makasino na kumbi kubwa za starehe. Bwana Matole anapenda sana kumaliza haja zake za kimwili na watoto wazuri kwenye kasino moja kubwa la kimataifa liitwalo. Merinde Cassino lililopo katikati ya jiji hili la Sami ado, ukimkosa hapo utamkuta kwenye kasino la New Angel au kwenye Hoteli kubwa maafuru hapa nchini."
"Merinde Casino, naijua hata hizo nyingine hivyo naweza kukutana naye tukazungumza mawili matatu."
"Naam." Alijibu Bwana Aziz kisha akapiga tarumbeta chupa yake kisha akairejesha mezani tena.
"Huyo Mr. Wasika Jerome upotevu wake haukuwahi kuchunguzwa?" Aliuliza Roi huku akijifuta mikono yake kwa tishu alitoshelezwa tayari kwa kilaji na nyama choma. Hakutaka tena kuendelea kunywa kwani kinywaji kilikuwa hakipandi kabisa hasa alipoambiwa habari za rafiki yake Frank Matiale. Mtu anayetoa msaada mkubwa sana hasa anapojua ndani yake anafanya kazi na majasusi tokea Tanzania.
TUKUTANE TENA JUMA TATU KWA SEHEMU YA NNE.