
16/12/2024
YESU SI MUNGU:
KWA SABABU MUNGU NI MMOJA TU.
Baadhi ya Wakristo wanatafuta sababu na udhuru wa kumfanya Yesu kuwa Mungu. Kwa mfano husema kwamba Yesu ni Mungu au mwana wa Mungu au Yesu ni Mungu mdogo au Yesu ni nafsi moja ya Mungu. Mambo haya yote ni kufuru tupu iliyovuka mipaka. Kwa sababu sawa na Biblia Mungu ni mmoja tu. Hakuna Mungu mdogo wala Mungu mwana. Biblia inasema:-
1. Wewe naam, wewe peke yako ndiye Mungu wa falme zote za dunia; wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. (2 Wafalme 19:15).
2. Kwa kuwa ndiwe mkuu, wewe ndiwe mfanya miujiza, ndiwe Mungu peke yako. (Zaburi 86:10).
3 Na uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma, (Yohana 17:3).
Sasa wakati Mungu wa pekee ni mmoja, hivyo Mungu zaidi ya mmoja ni wa uwongo.
4. Mwawezaje kuamini ninyi, mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti? (Yohana 5:44).
5. ...Hakuna Mungu ila mmoja tu. Kwa maana ijapokuwa wako waitwao miungu, ama mbinguni au duniani; k**a vile walivyoko miungu mingi na mabwana wengi. Lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu. aliye baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake. (1 Wakorintho 8:4-6).
Sawa na aya hizi hakuna Mungu ila mmoja tu. Ingawa miungu wa bandia wanatajwa tajwa mbinguni na ardhini. Basi sasa ambaye anaamini mungu minghairi ya Mwenyezi Mungu anatoka katika imani na anaingia katika ushirikina kwa sababu ya kuwaita miungu zaidi ya mmoja ambaye ni wa kweli na wa pekee.
6. ..Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu. (Marko 2:7).
Aya hii inathibitisha kwamba mwenye kufuta na kuondoa dhambi ni mmoja tu ambaye ni Mungu. Yaani hakuna mungu wa pili wala wa tatu wala mwenye kufuta dhambi isipokuwa Mwenyezi Mungu tu. Siyo aya hizo tu, bali tunaposoma Biblia tunakuta msululu wa aya kadhaa ambazo zinataja umoja wa Mungu. Kwa mfano: Kumbukumbu 4:39, 6:4; Nehemia 9:9; Isaya 43:10-11; 44:6-8, 44:5. 45:21-22, 46:9; Marko 12:32; Luka 18:19; Mathayo 4:10; Warumi 3:30; Timotheo 1:17, 2:5.
Hakuna aya hata moja inayosema kwamba Yesu ni Mungu..
Na Mw/Ally Muhammad Kaswezi.