07/05/2025
RAMALLAH, Mei 7, 2025 (WAFA) – Ramzi Khouri, mjumbe wa Kamati Kuu ya Utendaji ya PLO na mkuu wa Kamati Kuu ya Rais ya Masuala ya Kanisa nchini Palestina, ametuma wito wa dharura kwa mapatriaki na viongozi wa makanisa kote duniani, akiwataka wachukue hatua za haraka na madhubuti kulinda uwepo wa Wakristo katika Ardhi Takatifu kufuatia kuongezeka kwa ukiukwaji unaofanywa na utawala wa Israel.
Katika ujumbe wake, Khouri ameonya kuwa sera za sasa za Israel zinalenga kufuta kabisa uwepo wa Wakristo Wapalestina, kuwanyima haki zao za msingi za kidini na kitaifa, pamoja na kutenda ukatili mkubwa dhidi ya maeneo matakatifu. Ametaja vitendo hivyo kuwa ni pamoja na kufurushwa kwa lazima, mauaji, na kampeni ya utakaso wa kikabila maeneo mbalimbali ya Palestina, kuanzia Yerusalemu, Ukingo wa Magharibi hadi Ukanda wa Gaza ulioko chini ya mzingiro.
Barua hiyo imeangazia vikwazo vikubwa vilivyowekwa wakati wa Sikukuu ya Pasaka na Jumamosi Kuu mwaka huu. Khouri amesema kuwa siku ya Jumamosi Kuu, mamlaka ya Israel iligeuza jiji la Yerusalemu kuwa eneo la kijeshi, na kuwazuia maelfu ya waumini wakiwemo makasisi, mahujaji na hata mabalozi kuingia Kanisa la Kaburi Takatifu. Tukio la kushangaza lililotajwa ni la Askofu Mkuu Adolfo Tito Yllana, balozi wa Vatican kwa Palestina, ambaye alinyimwa ruhusa ya kuingia, jambo lililotafsiriwa k**a fedheha isiyokuwa na mfano na ishara ya hatua ya hatari ya kufuta utambulisho wa Kikristo wa Yerusalemu.
Kamati hiyo pia imelalamikia kampeni ya makusudi inayokiuka uhuru wa kuabudu. Imesema ni waumini 1,800 tu kati ya zaidi ya 50,000 Wakristo Wapalestina kutoka Ukingo wa Magharibi walioruhusiwa kuingia Kanisa la Kaburi Takatifu mwaka huu tofauti kubwa na kawaida ya waumini zaidi ya 10,000 wanaoshiriki Pasaka kila mwaka. Wengi walikumbwa na vikwazo au unyanyasaji katika vizuizi vya kijeshi vilivyokuwa vikali zaidi.
Zaidi ya hayo, Israel imeweka ushuru mkubwa usio halali dhidi ya taasisi za Kanisa huko Yerusalemu, ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kihistoria ya kidini. Barua hiyo pia imeeleza matukio ya mara kwa mara ya mashambulio dhidi ya makanisa na alama za kidini za Kikristo, na kuonya kuwa hali hii ni tishio la moja kwa moja kwa urithi wa kidini na kitamaduni wa Wakristo jijini humo.
Ujumbe wa Khouri umebainisha kuwa ukiukwaji huu ni sehemu ya mkakati mpana wa kuwafurusha Wapalestina, kuwapokonya haki zao, na kuzuia kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina lenye Yerusalemu k**a mji mkuu wake. Pia ameelezea janga la kibinadamu linaloendelea Gaza, ikiwa ni pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu na taasisi za Kanisa, na kufurushwa kwa karibu familia zote za Kikristo hadi kwenye maeneo ya makanisa.
Kamati hiyo imetoa wito kwa viongozi wa makanisa duniani kuchukua msimamo wa wazi na wa kishujaa katika kutetea haki za Wapalestina. Imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuishinikiza serikali ya Israel kusitisha ukiukwaji wake, kulinda maeneo matakatifu, kuhakikisha uhuru wa kuabudu, na kuiwajibisha Israel kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Barua hiyo inahitimishwa kwa maneno haya: kimya hakiwezi kuvumilika tena huu ni wakati wa kusema ukweli na kuchukua hatua ya ujasiri.