11/12/2025
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, M***a Azzan Zungu, ametangaza kifo cha Mbunge wa Peramiho, Jenista Joakim Mhagama, kilichotokea leo Alhamisi, Desemba 11, 2025 jijini Dodoma.
Katika taarifa yake, Spika Zungu amesema:
“Kwa masikitiko makubwa, naomba kutangaza kifo cha Mbunge wa Peramiho Mheshimiwa Jenista Mhagama kilichotokea leo 11 Desemba, 2025 jijini Dodoma. Natoa pole kwa waheshimiwa Wabunge wote, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa Jimbo la Peramiho. Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.”
Jenista Mhagama, alizaliwa Juni 23, 1967, na amehudumu katika nafasi mbalimbali ndani ya Serikali na Bunge la Tanzania, akiacha mchango mkubwa katika utumishi wa umma.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bunge, ofisi hiyo inashirikiana na familia ya marehemu kuratibu taratibu za mazishi, na taarifa zaidi zitatolewa kadiri mipango itakavyokamilika.
“Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, amina,” imehitimisha taarifa hiyo.