29/06/2025
“UNAKUFA KATIKA UMRI WA MIAKA 20 UNAZIKWA UKIWA NA MIAKA 60’’
Nilikuwa nasoma kitabu kimoja nikakutana na sentensi hii, ikanifikirisha kidogo.
Nikataka kujua mwandishi wa kitabu hicho alimaanisha nini kusema watu wengi hasa Afrika, wanakufa wakiwa na miaka 20 lakini wanazikwa wakiwa na miaka 60?
Katika kujifunza zaidi nikagundua tabia 08 zinazoweza kuonyesha mtu aliyekufa lakini angali na uhai ndani yake.
1. Kuamka na kulala bila ratiba maalumu.
Hii ni tabia inayowakumba vijana wengi wasomi na wasio wasomi. Utamkuta mtu na familia yake kabisa lakini anaamka asubuhi anajiuliza au anasemezana na mwenzake leo sijui niende wapi, sijui nifanye nini!
Utasikia oyaa! Una mchongo wowote huko?
Akiambiwa hakuna anarudi kulala asubirie chai au ugali wa mchana.
2. Kutoishi katika uhalisia.
Hii ni tabia waliyo nayo vijana wa kitanzania.
Kupenda kumiliki vitu vya kujionesha visivyoendana na uhalisia wa maisha yao.
Mathalani mtu yuko radhi auze mtaji wake wote wa kuku ili amiliki iPhone. Pasipo kujua atapoteza zaidi kuliko kuingiza faida.
3. Kutojua kusudi lako kuwepo duniani.
Kuna watu utasikia anasema “Kikubwa uzima mengine tumwachie Mungu’’
Hiyo ni tabia inayoonesha umekufa lakini una pumzi ndani yako.
Kila mwanadamu hakuzaliwa na nguo, na sio wote walizaliwa wakakuta pesa.
Wengi wamekulia katika mazingira magumu lakini kwa kuwa walijua kusudi lao la kuumbwa wamemiliki mali na wanazidi kuongeza zaidi.
Kumbe tunahitaji kuchukua hatua kila siku, pasipo kukata tamaa, maana mtafutaji hachoki na akishachoka ujue kapata.
4. Kuiga maisha ya wengine.
Utasikia “aisee jamaa kanunua friji na mimi nanunua friji” unachukua mtaji wako wa samaki unanunua pasipo kujua mwenzako kanunua kupitia faida aliyoingiza katika biashara yake.
Utajikuta mpaka unakufa, ulikuwa mtu wa kufukuzia mafanikio ya watu wengine wakati malengo yako na kusudi la Mungu kukuweka duniani haujalitimiza.
5. Kutowajibika katika majukumu yako.
Hapa nirukie kwa wanafamilia.
Wewe ni baba au mama hauwajibiki katika kutunza familia wakati unajua familia ni baraka kutoka kwa Mungu, wewe umekufa angali una pumzi.
Kwa sababu mtu asiye tunza familia ni zaidi ya mchawi.
Familia imetoka kiunoni mwako mwenyewe, unashindwaje kuwapa watoto mavazi na mazingira bora ya Elimu ili hali wewe umesomeshwa na wazazi wako na una mshahara?
Familia yako inapoadhirika jua wazi uko uchi, yaani sehemu zako za siri ziko wazi.
K**a unavyokuwa makini kuzilinda sehemu nyeti za mwili wako ndivyo unavyotakiwa kuwatunza wanao maana wametoka huko.
6. Kung’ang’ania jambo lisilo kupatia faida.
Utakutana na kijana na nguvu zake kabisa anashinda stendi kuokota hamsini hamsini anazotupiwa na makondakta.
Akisha kusanya 1500 ananunua msosi anavutia sigara, siku imeisha.
Akirudi nyumbani harudi na chochote anadai chakula kwa mkewe, pesa hajapeleka anakula analala.
Mtu wa namna hii hayupo katika kundi la watu wanaoishi labda wanaopumua.
Tunamtofautishaje na waliolazwa wakipumulia mashine?
7. Hurka ya matumizi mabaya ya pesa.
“Hebu tutumie tu pesa yote, ya kesho yatajisumbukia au wewe una
uhakika wa
kufika kesho?”
Mtu k**a huyu kwa vyovyote vile huwezi kusema ana maisha ndani yake.
Tabia ya mtu anayejua kusudi la kuishi lazima awe mtunza akiba na nidhamu katika matumizi ya pesa.
Wapo watu wengi wamejikuta wakiishi maisha ya kukimbia nyumba zao kwa sababu ya madeni yaliyozidi kipimo.
8. Kukata tamaa na kupuuzia kila jambo.
Kuna mtu utamshauri fanya hivi, atakujibu mbona hata fulani alijaribu akashindwa, mimi ni nani hata nifanikiwe?
Huyu mtu tayari amejikatia tamaa na hawezi kufika popote tena maana mawazo yake hayapo katika kutafuta njia mbadala za kufikia mafanikio au kujifunza kwanini wale walifeli na yeye atumie njia gani afanikiwe.
Mwingine anasema Mungu mbona unakawia njoo unichukue.
Unampangia Mungu ratiba ndo hakuchukui sasa mpaka unafikia miaka 60 ya kifo chako, umezaa watoto 10 lakini una vyumba viwili na sebule tu.
Tuache kujikatia tamaa, kuona hatuwezi ili hali kila mtu kaumbwa na kaletwa duniani kwa kusudi maalumu.
Kwanini unakata tamaa wakati tunaambiwa kibaiolojia mbegu zaidi ya milioni mia hukimbia kuelekea mfuko wa uzazi, lakini ni moja tu hufaulu na kutengeneza mtoto ambaye ni wewe.
Tafsiri tu ni kwamba umezaliwa kuwa mshindi na unatakiwa ushinde.
Ushindi upo katika kuishi vile unatakiwa kuishi k**a kusudi la Mungu linavyokutaka. Kutobweteka bali kwa kuwajibika ili kujiletea maendeleo
Mungu hakukuumba uwe maskini.
Tambua Fursa, kimbilia fursa.
Ukimbie umasikini kwa mbio kubwa