14/10/2022
MBUNGE SAGINI ATOA MAAGIZO MGOGORO WA MPAKA ULIODUMU MIAKA 34
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini amemuagiza Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara kuharakisha uchunguzi na kuchukua hatua za haraka kwa wote watakaobainika kuhusika katika mauaji ya Mzee Omary Iyombe (64) Mkazi wa Kitongoji cha Kwigina Kijiji cha Kizaru Kata Muryaza wilayani Butiama.
Maagizo hayo ameyatoa mapema hii leo aliposhiriki katika mazishi ya marehemu Mzee Iyombe aliyeuawa mnamo Septemba 24, 2022 akiwa anatoka sokoni Majira ya asubuhi, kuvamiwa kisha kushambuliwa kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili, kisa kikiwa ni mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda wa takriban miaka 34.
"Jeshi la Polisi linaendelea na misako na upelelezi mpaka tuwajue waliofanya mauaji haya na pia nilipata taarifa kuwa mlianza kufyekana asubuhi baada ya tukio hili kutokea, wakati serikali iliwapa muda wa wiki moja kuja kusikilliza pande zote mbili, hivyo hatuwezi kuvumilia vitendo hivi vinavyoendelea kutokea katika Wilaya Takatifu ya Butiama," amesema Mhe. Sagini.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Muryaza Dismas Maila amewaomba wananchi na familia kiujumla kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu na ndio maana Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amefika kwa haraka ili haki ipatikane.
Aidha Mwenyekiti wa Kijiji cha Kizaru Kennedy Juma, ameeleza kuwa mgogoro wa muda mrefu wa mpaka dhidi ya Kijiji cha Kizaru na wenzao wa Kijiji cha Kamgendi ndio chanzo cha watu kuuana kwani wenzao wamekuwa wakikataa maamuzi ya serikali kuhusu mpaka huo na pia wamefikia hatua hadi ya kutishiwa kwenda kijiji hicho kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kimaendeleo japo wote ni watanzania.
Ofisi ya Mbunge Butiama Kitengo cha Habari