15/04/2025
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limetoa ufafanuzi wa picha mjongeo (video clip) iliyoonekana kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikihusisha watu waliokuwa wanatumia gari lenye namba za usajili T.540 EHF aina ya Toyota Noah ikidaiwa walikuwa wakijaribu kumteka kijana mmoja aitwaye Jonathan Ayo (37), mkazi wa KCMC Moshi eneo la Mbuyuni Wilaya ya Moshi Manispaa Aprili 12, 2025.
Taarifa ya leo Aprili 14, 2025 iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoani humo imeeleza kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo Jeshi hilo lilifanya ufuatiliaji mara moja na kufanikiwa kuwak**ata watu wawili ambao ni Kelvin Temu (39), mkazi wa KCMC Moshi na Samson Magere (30), mkazi wa Soweto Moshi wakiwa na gari T.540 EHF aina ya Toyota Noah inayodaiwa kuhusika katika tukio hilo ambapo Gari hilo linamilikiwa na Kampuni ya KESSA TOURS yenye ofisi zake mtaa wa Soweto Moshi Mjini.
Uchunguzi wa tukio hilo umebaini kwamba tukio hilo halikuwa la utekaji bali Watuhumiwa hao walikuwa wamemuajiri Jonathan Ayo anayedaiwa kutekwa k**a mtaalam wa mifumo (I.T) wa kampuni yao ambapo tarehe 06 Aprili, 2025 alikwenda ofisini kwao mtaa wa Soweto kuchukua kompyuta mpakato (Laptop) ya ofisi akieleza kuwa anataka kufanyia kazi za ofisi akiwa nyumbani kwake na angeirudisha kesho yake.
Baada ya Ayo kuondoka na laptop hiyo hakuirudisha ndipo waajiri wake walipata mashaka na walianza kumtafuta kwa siku tano bila mafanikio. Ilipofika tarehe Aprili 12, 2025 walifanikiwa kumpata akiwa Bar mtaa wa Rau akinywa pombe ambapo alikubali kwenda kuwakabidhi laptop hiyo na alifanya hivyo.
Watu hao wakitumia gari T.540 EHF aina ya Noah baada ya kuipata laptop yao waliamua wampeleke Polisi ndugu Ayo kwa hatua zaidi na walipofika eneo la Mbuyuni majira ya saa moja usiku Ayo alifungua mlango wa gari ikiwa imesimama kwenye foleni na kujaribu kukimbia akiwa anapiga kelele za wezi zilizopelekea Wananchi kuwashambulia watu hao ambapo Askari Mgambo aliyekuwa eneo hilo alifanikiwa kuzuia vurugu hizo na kumfikisha Ayo kituo cha Polisi Moshi.