12/11/2025
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeendesha mafunzo kwa makundi mbalimbali mkoani Mtwara, ikiwemo walemavu, wanawake na wajasiriamali, kuwajengea uwezo wa kuchangamkia fursa za tenda zinazotangazwa na serikali kupitia idara za ununuzi.
Akifungua mafunzo hayo katika Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bahati Geuzye, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwani yanawawezesha wadau hao kuelewa vyema sheria, kanuni na taratibu za ununuzi wa umma.
Geuzye amesema zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya serikali hutumika kwenye ununuzi wa umma, hivyo ni muhimu kwa wananchi wote wenye sifa kushiriki na kunufaika na miradi ya maendeleo kupitia mifumo rasmi ya serikali.
“Tunaishukuru PPRA kwa fursa hii, kwani mafunzo haya yataleta uelewa na kutoa nafasi sawa kwa makundi yote kushiriki katika tenda za serikali,” alisema Geuzye.
Kwa upande wake, mwakilishi wa PPRA, Magnus Steven, ameeleza mafunzo hayo yalianza Novemba 10, 2025 katika Manispaa ya Mtwara-Mikindani na yataendelea katika halmashauri zote tisa za mkoa huo.
Amesema yanalenga kutoa elimu juu ya sheria na kanuni za ununuzi wa umma pamoja na namna ya kutumia mfumo wa kielektroniki wa manunuzi (NeST) ili kurahisisha ushiriki wa wananchi.
Baadhi ya washiriki, akiwemo Fatuma Mpondomoka, wameishukuru serikali kwa kuwajengea uwezo huo, wakisema elimu hiyo itawawezesha kushiriki ipasavyo katika zabuni za serikali.
Mwingine, Mustafa Yasini, amesema kupitia mfumo wa NeST sasa wataweza kufuatilia na kushiriki kikamilifu katika fursa mbalimbali za ununuzi wa umma.