16/03/2020
Serikali ya Tanzania imetangaza kuwa, tayari imechukua hatua kadhaa za tahadhari ili kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya Corona na kwamba kwa sasa nchi iko salama.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt Hassan Abbasi wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari.
Amesema kuwa, serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha virusi hivyo vya corona sio tu haviingii nchini, lakini pia kuzuia kusambaa kwa maambukizi endapo vitaingia.
“Zipo hatua zinazochukuliwa ndani ya taasisi na wizara moja moja, lakini pia zipo hatua za kitaifa za kukabiliana na virusi hivyo, na hivyo naomba kuwatoa hofu Watanzania kuhusu Corona” amesema Dkt. Abbasi.
Njia muhimu za kujinga na virusi vya Corona
Aidha ametaja miongoni mwa hatua hizo kuwa ni ile ya serikali kuandaa utaratibu maalumu katika maeneo ya viwanja vya ndege na maeneo ya mipakani, ambapo watu hawapimwi homa ya corona bali joto la mwili ili kuangalia endapo joto limezidi kiwango cha kawaida cha binadamu.
Wakati nchini Tanzania hali ya mambo ikiwa hivyo, Serikali ya Rwanda imethibitisha kesi nyingine nne za maambukizi ya virusi vya Corona na kufanya idadi ya kesi hizo kufikia tano.
Nchi Kenya pia, jana kulithibitishwa kesi mbili mpya za virusi vya Corona katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Rais Kenyatta ameagiza kufungwa kwa shule zote za kutwa nchini humo kuanzia leo Jumatatu, huku shule za bweni zikipewa hadi Jumatano kutekeleza agizo hilo. Aidha Vyuo Vikuu na taasisi za elimu za juu nchini humo zimetakiwa kufungwa kufikia Ijumaa ijayo