31/05/2026
MJUMBE WA BARAZA KUU LA UVCCM TAIFA, SAMEER MURJI, AZUNGUMZA NA WANACHAMA WA CCM BEIJING, CHINA
Beijing, China – 31 Mei 2026
Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Sameer Murji, leo ameshiriki Mkutano wa Nusu Mwaka wa Shina la CCM Beijing uliofanyika jijini Beijing, China, ambapo alipata fursa ya kuzungumza na wanachama wa CCM pamoja na Watanzania wanaoishi nchini humo.
Akizungumza katika mkutano huo, Sameer Murji amewapongeza viongozi wa Shina la CCM Beijing kwa kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na ushiriki wa wanachama katika shughuli za chama licha ya kuwa nje ya Tanzania.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa Watanzania waliopo China kutumia fursa za elimu, biashara, teknolojia na uwekezaji zinazopatikana nchini humo kwa manufaa ya maendeleo ya Tanzania.
“Nimefurahishwa sana kuona jinsi ambavyo wanachama wa CCM Beijing wameendelea kuwa wamoja na kushirikiana. Raha ya mwana CCM ni kukutana, kufahamiana na kusaidiana katika safari ya maendeleo ya Taifa letu,” alisema Murji.
Katika hotuba yake, Murji ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi na mahusiano ya kimataifa ambayo yameendelea kufungua fursa mbalimbali kwa Watanzania ndani na nje ya nchi.
Pia ameeleza kuwa mahusiano kati ya Tanzania na China yanaendelea kuimarika na kutoa rai kwa vijana wa Kitanzania waliopo China kutumia maarifa na uzoefu wanaoupata kuchangia maendeleo ya Taifa pindi wanaporejea nyumbani.
Vilevile, amewahimiza Watanzania waliopo China kuendelea kusaidiana, kushirikiana na kuinuana katika nyanja mbalimbali za maendeleo huku wakibaki kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania.
Sameer Murji yupo nchini China kwa kushiriki Seminar for Youth Cadres from Belt and Road Countries, programu ya mafunzo ya vijana viongozi inayowakutanisha washiriki kutoka nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika masuala ya maendeleo, uongozi na ushirikiano wa kimataifa.
Updates
Mtwara Online Tv
Habari Kiganjani Kwako