
04/07/2025
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bi. Bahati Geuzye amelipongeza shirika lisilo la kiserikali la Door of Hope lililopo Mkoani Mtwara, kwa kufanya utatuzi wa mashauri 131 na kufikia wananchi 6,735.
Akizungumza katika kikao cha mrejesho wa shughuli za huduma za msaada wa kisheria mkoani Mtwara, uliotolewa na Vikosi kazi vya Msaada wa kisheria kutoka Wilaya ya Mtwara na Tandahimba kilichofanyika leo Julai 4,2025 katika ukumbi wa Veta Manispaa ya Mtwara Mikindani, Bi Geuzye amewataka waendelee kutoa elimu kwa jamii ili kuisaidia Serikali kupunguza migogoro inayopelekea masuala ya ukatili wa kijinsia.
Aidha Bi Geuzye ametoa rai kwa shirika hilo kuhakikisha wanawafikia wananchi wa maeneo ya wilaya za pembezoni, ili kukuza wigo wa kutoa huduma hizo za msaada wa kisheria ambazo zimekuwa kikwazo kwa wananchi hususan wa vijijini.
Kwa upande wake Betilda Rwakatale ambaye ni Mwanasheria wa shirika la Door of Hope mkoani Mtwara, akizungumza Kwa niaba ya Mkurugenzi wa shirika hilo amesema wamefanikiwa kufikia wananchi hao 6,735 katika kata Saba, tatu kutoka Wilaya ya Mtwara na Nne kutoka wilaya ya Tandahimba, huku migogoro mingi ikihusu masuala ya Ndoa.