16/04/2025
Wizara ya TAMISEMI imesema kupitia ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP) imefanikisha hatua ya kihistoria ya kusaini mikataba na watoa huduma watatu wa uendeshaji wa awamu ya pili ya mabasi yaendayo haraka ambapo imesema mabasi hayo yatapunguza foleni za Dar es salaam na kuharakisha uchumi.
Akiongea leo April 16,2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati wa hotuba yake kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2025/2026, Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amesema “Kwa muda mrefu Watu wa Jiji la Dar es salaam wamekuwa wakisubiri, wengine kwa matumaini, wengine kwa mashaka lakini wote kwa kiu ya mabadiliko, leo kwa mara ya kwanza tunasema, subira yao haikuwa ya bure, kupitia ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP), tumefanikisha hatua ya kihistoria kusaini mikataba na watoa huduma watatu wa uendeshaji wa awamu ya pili ya mabasi yaendayo haraka”
“Hili ni tukio la mwanzo wa zama mpya siyo tena hadithi ya ahadi zisizotekelezwa, bali ya huduma bora zinazoonekana na kuguswa ‘Great things take time’, Wanafalsafa wanasema, ‘Mambo makubwa yanahitaji muda’ hatua hii si tu ununuzi wa huduma, bali ni ununuzi wa matumaini mapya kwa wakazi wa Jiji letu, hatutaki kurudia makosa ya jana, bali tunajenga mfumo imara, unaozingatia ubora, ufanisi na heshima kwa muda na maisha ya abiria”
“Hope is being able to see that there is light despite all the darkness’ – Desmond Tutu, kwa miaka mingi Wananchi wamepitia usumbufu, foleni zisizokwisha na huduma zisizoeleweka lakimi, tunasema kwa sauti ya matumaini, nuru inaanza kuonekana, mabasi haya hayatakuwa tu magari ya kusafirisha Watu, yatakuwa magari ya kusukuma uchumi, kuunganisha fursa na kupunguza mzigo wa maisha ya kila siku, ‘Progress is not in enhancing what is, but in advancing toward what will be’ – Khalil Gibran.
“Mradi huu unaonesha jinsi tunavyotoka kwenye kilichozoeleka foleni, ajali, uchakavu na kuelekea kwenye kile kinachowezekana, usafiri wa kisasa, wa heshima, wa watu wote, tunajenga mfumo wa usafiri wa umma ambao utaweka heshima kwa abiria, uwajibikaji kwa watoa huduma na thamani kwa kila senti inayowekezwa”