13/05/2026
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imetoa onyo la mwisho kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kikitakiwa kuwasilisha maelezo ya utetezi kwanini usajili wake usisimamishwe kufuatia tuhuma za ukiukwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa.
Katika barua rasmi ya Mei 7, 2026, yenye kumbukumbu namba HA.322/362/16A/22, Msajili amebainisha kuwa CHADEMA imekuwa ikitumia lugha za kashfa, uchochezi, na dhihaka zinazoweza kuhatarisha usalama wa taifa na utulivu wa nchi kupitia viongozi wake na matamko ya Kamati Kuu.
Msajili amewasilisha malalamiko dhidi ya kauli za viongozi wa chama hicho, akiwemo Makamu Mwenyekiti (Bara), John Heche, kuhusu mpango wa kuitisha maandamano kushinikiza kuachiwa kwa Tundu Lissu. Msajili amedai kuwa hatua hiyo ni kuingilia uhuru wa Mahak**a na kuchochea uvunjifu wa amani.
Aidha, barua hiyo imemnukuu Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Korogwe, Oliver Kisaka, akituhumiwa kutoa matamshi yanayohamasisha matumizi ya nguvu k**a njia ya kufikia malengo ya kisiasa, jambo ambalo ni kinyume na Kifungu cha 19(2)(c) cha Sheria ya Vyama vya Siasa.
Hoja nyingine nzito ni tamko la Kamati Kuu ya CHADEMA la Mei 5, 2026, ambalo Msajili amedai lina lugha za kashfa dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan na vyombo vya dola. Msajili amekosoa madai ya chama hicho kuwa Serikali "imetwaa madaraka kwa mabavu" na "mtutu wa bunduki," akisisitiza kuwa kauli hizo ni batili na zinadhalilisha taasisi ya Urais.
CHADEMA imepewa hadi Mei 20, 2026, saa tisa na nusu alasiri, kuwasilisha utetezi wake. Msajili ameonya kuwa endapo maelezo hayo hayatatosheleza, chama hicho kinaweza kukabiliwa na rungu la sheria ikiwemo kufutwa kwa usajili, kutozwa faini, au kuzuiwa kufanya baadhi ya shughuli za kisiasa kwa mujibu wa Sheria Namba 3 ya Mwaka 2024.