30/12/2025
Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, leo Jumanne tarehe 30.12.2025, amewapa Daraja la Ushemasi Jumla ya Mafrateri 13 wa Jimbo.
Misa ya utolewaji wa Daraja la Ushemasi imefanyika katika kanisa kuu la Mama mwenye Huruma Ngokolo mjini Shinyanga, na imehudhuriwa na Mapadre, watawa na waamini kutoka sehemu mbalimbali za ndani na nje ya jimbo.
Askofu sangu amewahimiza waamini kuendelea kuwaombea Mashemasi hao ili Mungu roho Mtakatifu awaongoze katika utume wao.
Aidha, amewataka Mashemasi hao kutambua kuwa, wameacha yote ikiwemo maisha ya ndoa kwa ajili ya kazi ya Mungu, hivyo wakawe walimu waaminifu wa neno la Mungu na kielelezo cha Imani kwa watu.
Mashemasi hao wapya ni Boazi Madundo kutoka Parokia ya Nyalikungu, Charles Mahembo wa Parokia ya Gula, John Mkama wa Parokia ya Buhangija, Joseph Solo wa Parokia ya Maganzo, Nicholaus Masele wa Parokia ya Old Maswa, Nobert Nyabahili wa Parokia ya Malampaka, Paschal Jilala wa Parokia ya Shishiyu na Severino Komanya wa Parokia ya Mwanangi.
Wengine ni Shemasi Simon Masolwa kutoka Parokia ya Shishiyu, Stephen Seso wa Parokia ya Malampaka, Sylvester Masano wa Parokia ya Nyalikungu, Valerian Maziku wa Parokia ya Mipa na Yusto Mrosso wa Parokia ya Mwamapalala.
Askofu Sangu ametangaza kuwapa Daraja takatifu la Upadre Mashemasi wote 13 mnamo Julai 16 mwaka 2026.