06/07/2025
ARSENAL WAKARIBIA KUKAMILISHA USAJILI WA VIKTOR GYOKERES KUTOKA SPORTING CP.
Klabu ya Arsenal iko katika hatua za mwisho za mazungumzo na Sporting CP kwa ajili ya kumsajili Mshambuliaji wa Sweden, Viktor Gyökeres, kwa mkataba wa miaka mitano hadi 2030. Kwa mujibu wa Mwandishi wa habari za michezo, Ben Jacobs, pande zote mbili zinamatumaini ya kufikia makubaliano ya mwisho hivi karibuni.
"Arsenal wanataka kufanya jambo moja: kumsajili Gyökeres au Sesko kwa €70m," alisema Ben Jacobs katika mahojiano na Tribuna.
Gyökeres, mwenye umri wa miaka 27, alifunga mabao 54 katika mechi 52 msimu uliopita, akiisaidia Sporting CP kutwaa taji la Primeira Liga kwa mara ya pili mfululizo. Mchezaji huyo anatajwa kuwa na nia ya kujiunga na Arsenal, licha ya klabu k**a Manchester United na Chelsea pia kuonyesha nia ya kumsajili.
Sporting CP inadai ada ya uhamisho ya angalau £68.5 milioni, ambayo ni juu ya makubaliano ya awali ya £60 milioni ambayo klabu hiyo inakanusha kuwepo. Gyökeres amekataa ofa kutoka kwa klabu za Saudi Arabia, akisisitiza kuwa anataka kucheza Ligi Kuu ya England, hasa Arsenal.
Arsenal tayari imemsajili Kiungo wa kati, Martín Zubimendi, kutoka Real Sociedad kwa £51 milioni, na sasa inatafuta kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji kwa kumsajili Gyökeres.
Iwapo usajili huu utakamilika, Gyökeres atakuwa Mchezaji wa tatu ghali zaidi katika historia ya Arsenal, nyuma ya Declan Rice (£100m) na Nicolas Pépé (£72m).