
15/04/2025
JAJI MKUU ATAKA KASI ZAIDI MATUMIZI YA TEHAMA MAHAKAMANI
Asema kila mmoja atapimwa mfumo upi ametumia, kwa kiasi gani
Na FAUSTINE KAPAMA na ASHA JUMA-Mahak**a, Morogoro
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewahimiza Majaji na Mahakimu kote nchini kuongeza kasi ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHAMA- kwenye usikilizaji wa mashauri ili kufanya vizuri zaidi katika utekelezaji wa jukumu la utoaji haki kwa Wananchi.
Mhe. Prof. Juma ametoa wito huo leo tarehe 15 Aprili, 2025 alipokuwa anafungua Mkutano Mkuu wa Mwaka 2024 wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), ambao umefanyika mwaka huu 2025 katika Hoteli ya Morena mjini hapa.
‘Taarifa ya Msajili Mkuu katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi inaonesha kuwa mwaka jana 2024, sisi wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, tuliweza kumaliza mashauri mengi (mashauri 245,310) zaidi ya yale yaliyopokelewa (mashauri 242, 284),’ amesema.
Jaji Mkuu amewapongeza wanachama hao kwa mafaniko hayo makubwa katika kutimiza wajibu wao wa kikatiba k**a Mamlaka yenye Kauli ya Mwisho ya Utoaji Haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo, Mhe. Prof. Juma amebainisha kuwa Majaji na Mahakimu bado wanayo nafasi ya kufanya vyema zaidi endapo watajikita katika matumizi ya TEHAMA kwenye usikilizaji wa mashauri.
Amewakumbusha kuzingatia Waraka No. 1 wa Jaji Mkuu, ambao unaeleza kuwa uongozi utaanza kupima matumizi ya uwekezaji mkubwa ambao umefanyika kwenye mifumo mbalimbali ya TEHAMA.
‘Ni jambo moja kuwekeza kwenye mifumo ya TEHAMA na ni jambo tofauti kabisa k**a hatutumii kikamilifu. Fedha nyingi sana zimetumika katika kuwekeza kwenye mifumo hiyo. Sasa umefika wakati tuweze mwisho wa mwaka kujua nani ametumia mfumo upi na kwa kiasi gani ili tuone mapungufu yapo wapi tuweze kuboresha,’ Jaji Mkuu amesema.
Mhe. Prof. Juma amebainisha pia kuwa, kwa kutumia mifumo ya TEHAMA wanaweza kuhifadhi data kubwa ambayo imesheheni mambo mengi yanayoweza kuwasaiduia kujua kinachoendelea.