11/11/2025
MASOMO YA MISA, JUMANNE YA JUMA LA THELATHINI NA MBILI, KIPINDI CHA KAWAIDA, MWAKA I, KUMBUKUMBU YA MT. MARTINO WA TUR, ASKOFU, 2025
RANGI YA KILITURJIA: NYEUPE 🤍
SOMO LA KWANZA
HEKIMA YA SULEMANI 2:23—3:9
Machoni pa wapumbavu, walionekana k**a wamekufa.
Somo katika kitabu cha Hekima ya Sulemani
Mungu alimwumba mtu apate kutokuongoka; naye alimfanya mfano wake mwenyewe. Lakini kwa wivu wa Mwovu, kifo kiliuingia ulimwengu, na wale walioungana naye kushiriki mauti hayo. Lakini roho za wenye haki zi mkononi mwa Mungu, wala mateso yoyote hayatawagusa. Machoni pa wapumbavu walionekana k**a wamekufa; na kutoka kwao kulihesabiwa kuwa msiba; na kuondoka kwao toka kwetu kuwa uharibifu. Lakini wao wako katika amani. Na hata k**a kwa mtazamo wa watu, wanaonekana kuadhibiwa, tumaini lao limejaa kutokufa. Kwa kuadhibiwa kidogo, watafanyiwa mema makubwa, kwani Mungu aliwajaribu akawakuta kwamba wanamstahili yeye. Aliwatathmini k**a dhahabu katika tanuri, na k**a sadaka ya kuteketezwa aliwapokea. Na wakati wa kujiliwa kwao watang'aa, na wataruka huku na huko k**a cheche kwenye nyasi. Watawahukumu mataifa na kuwatawala watu, naye Bwana atakuwa mfalme wao hata milele. Wenye kumtumaini Mungu watafahamu ukweli, nao waaminio katika upendo watakaa naye, kwani neema na rehema ni kwa watakatifu wake, na ulinzi kwa wateule wake.
NENO LA BWANA... TUMSHUKURU MUNGU
ZABURI YA KUITIKIZANA
ZABURI 34:2—3, 16—17, 18—19 (K. 2a)
K. Nitamtukuza Bwana kila wakati.
Nitamtukuza Bwana kila wakati,
sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Nafsi yangu itajisifu katika Bwana;
wanyonge wasikie na kufurahi. K.
Macho ya Bwana yawaangalia wenye haki,
na masikio yake hukisikia kilio chao.
Uso wa Bwana ni juu ya watendao mabaya
ili afute Kumbukumbu yao duniani. K.
Wanyofu waliita, Bwana akasikia,
akawaponya katika shida zao zote.
Bwana yu karibu nao waliopondeka moyo,
huwaokoa wenye kuvunjika roho. K.
SHANGILIO LA INJILI
YOHANE 14:23
K. Aleluya. W. Aleluya.
K. Mtu akinipenda, atalishika neno langu, asema Bwana, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao kwake.
W. Aleluya.
SOMO LA INJILI
LUKA 17:7—10
Sisi watumishi wasio n faida; tumefanya tu tuliyopaswa kufanya.
† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Luka
Wakati ule: Yesu alisema, "Ni nani kati yenu, mwenye mtumishi wa kulima au kuchunga, atamwambia anaporudi kutoka shambani, 'Njoo mara, starehe?' Je, hatamwambia, 'Niandalie chakula, jifunge kanzu, nitumikie mpaka nitakapomaliza kula na kunywa, ndipo utakula na kunywa wewe?' Je, atamshukuru mtumishi kwa sababu amefanya aliyoamriwa? Nanyi pia, mkishafanya yote mliyoamriwa, semeni, 'Sisi ni watumishi wasio na faida; tumefanya tu tuliyopaswa kufanya.'"
INJILI YA BWANA... SIFA KWAKO EE KRISTO