
19/07/2025
Msanii mkongwe wa muziki wa Hip Hop Bongo, Professor Jay amekabidhiwa rasmi tuzo yake ya kimataifa kutoka Hollywood and African Prestigious Awards (HAPAwards), katika ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), jijini Dar es Salaam.
Makabidhiano hayo yaliongozwa hapo jana na Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa wa BASATA, Bwana Edward Buganga, aliyemkabidhi tuzo hiyo kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa BASATA, Dkt. Kedmon Mapana.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Prof. Jay alieleza furaha yake kwa kutunukiwa heshima hiyo kubwa na kimataifa, huku akiwashukuru mashabiki wake, wadau wa sanaa, na Serikali kupitia BASATA kwa kuendelea kumtambua na kumthamini.
“Kupokea tuzo hii nyumbani, mbele ya wasanii wenzangu na viongozi wa sanaa, ni heshima kubwa sana kwangu. Muziki wetu una thamani, na ninajivunia kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa,” alisema Prof. Jay kwa shukrani.
Kwa upande wake, Bwana Edward Buganga alitumia fursa hiyo kumpongeza Prof. Jay kwa ushindi huo na kuhimiza wasanii wengine kuendelea kufanya kazi kwa weledi na ubunifu ili kuvuka mipaka ya ndani na kufikia mafanikio ya kimataifa.