09/07/2026
Nyumba mbili za kifahari London zinahusishwa na Kiongozi Mkuu wa Iran zauzwa kwa mamilioni ya pauni.
LONDON, Uingereza.
Nyumba mbili za kifahari katika eneo la Kensington, London, zinazodaiwa kumilikiwa na Kiongozi Mkuu wa Iran, Mojtaba Khamenei, zimeanza kuuzwa baada ya Mfanyabiashara na Mwanabenki wa Iran, Ali Ansari, ambaye ametajwa kuwa Mtu muhimu wa mtandao wa kifedha wa Khamenei, kushindwa kulipa mikopo ya mali hizo.
Kwa mujibu wa ripoti ya The Sunday Times iliyochapishwa Septemba 6, 2026, nyumba hizo ziko katika jengo la 3a Palace Green, katika moja ya maeneo ya kifahari zaidi ya Kensington, na ziko umbali wa takribani mita 45 kutoka ubalozi wa Israel nchini Uingereza.
Mali hizo, zilizonunuliwa mwaka 2014 na 2016 kupitia Ansari, zina thamani ya pamoja ya takribani pauni milioni 35.75. Moja ilinunuliwa kwa pauni milioni 19 mwaka 2016 na sasa inauzwa kwa takribani pauni milioni 12, huku nyingine iliyonunuliwa kwa pauni milioni 16.75 mwaka 2014 ikiwa haina bei ya wazi ya kuanzia katika tangazo la mauzo.
Kila nyumba ina vyumba vya Wafanyakazi pamoja na eneo binafsi la juu la jengo, huku mali hizo zikiwa karibu na Kensington Palace, eneo linalohusishwa na makazi rasmi ya Prince na Princess of Wales.
- Uhusiano na mtandao wa Khamenei.
Uchunguzi wa awali wa Bloomberg umehusisha mali hizo na mtandao mpana wa uwekezaji unaodaiwa kuwa chini ya ushawishi au udhibiti wa Mojtaba Khamenei. Uchunguzi huo ulieleza kuwa mali kadhaa nchini Uingereza na sehemu nyingine za Ulaya zilisajiliwa kupitia Kampuni na watu wa kati badala ya kuwekwa moja kwa moja kwa jina la Khamenei.
Ansari ametajwa na vyanzo vya Magharibi k**a mmoja wa watu muhimu katika mtandao huo, lakini amekanusha vikali kuwa na uhusiano wowote wa kifedha au binafsi na Mojtaba Khamenei, kupitia Wakili wake.
- Mali hizo zafuatiliwa baada ya vikwazo.
Mamlaka za Uingereza zilimwekea Ansari vikwazo mwaka 2025, hatua iliyosababisha mali zake nchini Uingereza kuzuiliwa. Serikali ya Uingereza pia imethibitisha Bungeni kwamba hatua za vikwazo dhidi ya Ansari ziliathiri mali zake nchini humo, zikiwemo mali isiyohamishika.
Ripoti za hivi karibuni zinaeleza kuwa baada ya Ansari kushindwa kutimiza malipo ya mikopo ya nyumba hizo, mali hizo ziliingia katika mchakato wa receivership, na sasa zimewekwa sokoni. Fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo hayo zinatarajiwa kubaki chini ya masharti ya vikwazo wakati Ansari akiendelea kuwa kwenye orodha ya waliowekewa vikwazo.
- Eneo la nyumba hizo laibua maswali ya usalama.
Mahali zilipo nyumba hizo kumeongeza mvutano wa suala hilo kwa sababu ziko karibu sana na Ubalozi wa Israel Mjini London, ambao unalindwa kwa kiwango kikubwa kutokana na mazingira ya kiusalama.
Ripoti ya The Standard iliwahi kueleza kuwa Nyumba hizo zina mwonekano wa moja kwa moja kuelekea sehemu ya nyuma ya ubalozi, jambo lililoibua wasiwasi miongoni mwa Wataalamu wa usalama.
Kwa upande mwingine, uchunguzi wa Bloomberg umeonyesha kuwa suala la mali za London ni sehemu ya mtandao mpana zaidi wa uwekezaji unaodaiwa kuhusishwa na Khamenei, ukiwa na mali katika maeneo ya kifahari k**a Hampstead's “Billionaires’ Row” na maeneo mengine ya Ulaya na Mashariki ya Kati.
Mauzo hayo sasa yanaweka katika mtazamo mpana zaidi mjadala kuhusu jinsi mitandao ya watu wenye nguvu nchini Iran ilivyoweza kuwekeza katika mali za thamani kubwa katika nchi za Magharibi licha ya vikwazo vya muda mrefu dhidi ya Tehran.
Toa maoni yako