03/01/2026
Hujambo na karibu tena kweye vipindi vyetu vya DW Noa Bongo Jenga Maisha Yako katika mchezo unaoangazia Elimu ya Kidijitali. Ni kipindi cha Pili kwenye mfululizo wa mchezo wetu wa redio unaoitwa Suluhisho la Kidijitali. Hadithi hii inaelezea umuhimu wa kukuza elimu na ujuzi wa kidijitali unaohitajika kukabiliana na changamoto za kidijitali. Katika kipindi kilichotangulia, tulikutana na Faith, mwalimu wa shule ya Inzuna ambaye anaishi na binamu zake Rahim, na Jennifer. Rahim ametawaliwa na teknolojia ya habari na hutumia muda mwingi kwenye kompyuta yake. Jennifer hutegemea kipato chake kutokana na ubunifu wa ushawishi katika mitandao ya kijamii. Shule ya Inzuna, ambako Faith anafanya kazi, inashiriki katika shindano la ubunifu wa kidijitali baina ya shule chini ya maudhui Teknolojia ya Kidijitali katika sekta ya elimu.
Walimu wengi walishangaa kuona kuwa Faith ndiye aliyeteuliwa kuwa mratibu na kuwaongoza wanafunzi katika mradi huo wa shule kwenye shindano hilo, badala ya rafiki yake Nina. Licha ya kufurahia uteuzi huo, je, Faith anafahamu changamoto zake? Pia katika kipindi kilichopita, mama yake Jennifer aliwatembelea nyumbani kwao bila ya kutoa taarifa. Je ziara hii ya ghafla ilikuwa na ujumbe gani? Hebu tusikie yanayojiri katika kipindi hiki cha leo kwa jina Uvumbuzi. Tuskimalizie uhondo, jiunge nasi na utuandikie maoni yako!