18/07/2025
Chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kinachoegemea upande wa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kimewasilisha wagombea wake wa kwanza kushiriki katika chaguzi ndogo zijazo kwa ajili ya kujaza nafasi wazi za uongozi.
DCP kimemteua wakili Edgar Busiega kuwania kiti cha ubunge cha Malava, Kaunti ya Kakamega, na Aden Mohamed kuwania ubunge wa Banisa, Kaunti ya Mandera.
Kwa mujibu wa chama hicho, zaidi ya Wakenya milioni 1.8 tayari wamesajiliwa kuwa wanachama ndani ya muda wa miezi miwili tangu kuzinduliwa kwake.
Naibu kiongozi wa chama hicho, Cleophas Malala, alisema kuwa DCP itawasilisha wagombea katika kila uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika, ikiwemo maeneo yanayojulikana kuwa ngome za wafuasi wa Rais William Ruto.
“Tumeamua kuwa tutashiriki katika chaguzi ndogo zote nchini – viti vyote 22 vya MCA pamoja na viti sita vya ubunge. Hata katika eneo la Nyanza, tutatoa wagombea,” alisema Malala.
Aidha, Malala aliwataka makamishna wapya wa IEBC kuanza kazi mara moja kwa kuhakikisha uwazi, uwajibikaji, na uadilifu katika mchakato wa uchaguzi. Alisisitiza pia haja ya kuchukuliwa hatua kali dhidi ya viongozi waliodai kuwa uchaguzi wa mwaka 2027 utavurugwa.
“Tunaitaka IEBC ianze kuchukua hatua sasa. Tutaandikisha malalamiko rasmi dhidi ya wabunge waliotoa matamshi ya kuhatarisha amani kuhusu uchaguzi ujao,” alisema.