23/05/2025
Kakamega: Wenye Biashara ya Ngono Wateta Wadai Nyumba Kumi, Polisi Wanawasumbua.
āPolisi walitupiga na kututupa nje!ā Hicho ndicho kilio cha wafanyakazi wa ngono katika mji wa Kakamega, wanaodai kuwa wanakumbwa na unyanyasaji unaozidi kuongezeka kutoka kwa maafisa wa usalama na wale wa Nyumba Kumi nyakati za usiku wanapotekeleza kazi yao. Wanawake hao wamesema uvamizi unaodaiwa kufanyika kwa kisingizio cha kukusanya ushuru wa kila siku umegeuka kuwa wa vurugu, ukiwaacha na majeraha, mali iliyoharibiwa, na bila mahali pa kulala. Wakizungumza na wanahabari mapema hii leo mjini Kakamega, baadhi ya wenye biashara ya ngono walieleza jinsi wanaume waliovaa barakoa na nguo za kiraia ā wanaodaiwa kuwa polisi wanaoshirikiana na maafisa wa Nyumba Kumi ā walivamia vyumba vyao vya kupanga usiku wa manane, kuwacharaza, kuwaibia mali zao, na kubomoa makazi yao. āWalikuja saa sita usiku wakiwa wamevaa barakoa na nguo za kawaida, wakificha utambulisho wao. Walitupiga na kututupa nje kwa nguvu pamoja na magodoro yetu,ā alisema Sharon Kimangi, mmoja wa wanawake walioathirika. Sharon, ambaye sasa amekuwa sauti ya kundi hilo, aliongeza kuwa angalau wenzake 12 walikamatwa bila sababu wazi. Baadhi ya wanawake walipoenda katika Kituo Kikuu cha Polisi Kakamega kuuliza kuhusu kukamatwa kwao, walidaiwa kufukuzwa. āBaadhi yao walipigwa vibaya na kukamatwa. Lakini tulipojaribu kuwaona, tulinyimwa ruhusa na kuambiwa tuondoke,ā Sharon alilalamika. Aidha, alifichua kuwa baadhi ya waathiriwa walilazimika kulala nje baada ya nyumba zao kubomolewa na mali yao kulowana kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. Mwenye nyumba ambaye anapangisha baadhi ya wafanyakazi wa ngono alithibitisha uharibifu huo. Aliliambia wanahabari kuwa mali ya wapangaji wake ilitupwa nje na juhudi zake za kuzungumza na walioendesha operesheni hiyo zilipuuzwa. Wafanyabiashara ngono hao sasa wanaomba serikali iingilie kati, wakilaumu polisi waovu na maafisa wa Nyumba Kumi kwa kutumia nguvu kupita kiasi.
kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Kakamega Central, Vincent Cherutich, alikanusha madai hayo akisema operesheni hiyo ilikuwa inalenga kuwasaka wahalifu halisi mjini humo. āTunaendesha oparesheni ya kuwasaka wahalifu wa kweli. Ikiwa kuna afisa wetu aliyekiuka maadili, tutamchukulia hatua za kisheria,ā alisema Cherutich. Aidha, aliwataka maafisa wa Utawala wa Serikali Kuu (NGAO), wakiwemo machifu na manaibu wao, kuwabaini wahalifu wanaojifanya maafisa wa Nyumba Kumi kwa lengo la kuwatisha wananchi na kuwaibia.