
25/07/2025
Vinara wa Ligi ya Taifa Daraja la Pili Kanda ya Kaskazini ya Kundi A ya Shirikisho la Kandanda nchini Kenya (FKF) vijana wa Teita Estate FC ya kutoka Kaunti ya Taita Taveta, wikendi hii, wanacheza mechi mbili za ugenini katika Kaunti ya Kwale.
Kwanza Teita Estate FC wataanza kuwakabili wenyeji wao RWAFA FC kwenye Uwanja wa Nyumba Sita ulioko eneobunge la Msambweni Jumamosi hii ya Julai 26 kabla ya kumalizia kwa kuwavaa Denmark FC katika mechi ya mkondo wa pili itakayogaragazwa kwenye Uwanja wa Kombani ulioko eneobunge la Matuga siku ya Jumapili hii ya Julai 27, 2025.
Teita Estate FC, ambao waliwacharaza Denmark FC mabao 3-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza, wamejenga kibanda kileleni mwa jedwali ya ligi hiyo wakiwa na alama 67 baada ya kushuka dimbani mara 26 na kushinda mechi 21 wakitoa sare mechi nne na kupoteza mchezo mmoja.
Walifikisha alama hizo baada ya kupata ushindi wa nyumbani wa mabao 3-0 dhidi ya Mbungoni FC ya kutoka Kaunti ya Kilifi katika mechi iliyofanyika Uwanjani Alexander Complex Jumamosi ya Julai 20, 2025. Nao Denmark FC wanakamata nafasi ya tano kwa alama 52 wakati RWAFA FC ni ya nane ikiwa na alama 39.
Denmark FC waliwazaba Ziwani Youth FC ya Kaunti ya Mombasa mabao 2-0 katika mechi ya ugenini iliyochezwa kwenye Uwanja wa shule ya msingi ya Ronald Ngala (RG Ngala) Jumatano ya Julai 23, 2025.