23/08/2025
Ripoti iliyoidhinishwa na Umoja wa Mataifa na kutolewa jana (Ijumaa) imethibitisha kuwepo kwa njaa kali katika maeneo ya Ukanda wa Gaza, ikiwa ni mara ya kwanza njaa kutangazwa rasmi Mashariki ya Kati, jambo linaloongeza wasiwasi kuhusu hali mbaya ya kibinadamu katika eneo hilo lenye vita na athari za kisiasa zinazoweza kujitokeza.
Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Integrated Food Security Phase Classification (IPC), zaidi ya nusu milioni ya watu katika Ukanda wa Gaza, takriban robo ya wakazi wake, wamekumbwa na njaa kali, hasa jijini Gaza, huku janga likienea kusini hadi Deir al-Balah na Khan Younis. Ripoti pia imeonya kuwa hali Kaskazini mwa Gaza inakadiriwa kuwa mbaya zaidi.
“Hili ni janga lililotengenezwa na binadamu, ni shutuma ya kimaadili na ni kushindwa kwa utu wenyewe,” alisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, katika tamko lake jana (Ijumaa).
Kwa mujibu wa viwango vya IPC, eneo hutangazwa rasmi kuwa na njaa endapo vigezo vya juu vya ukosefu wa chakula, utapiamlo mkali na vifo vinavyohusiana na njaa vimevukwa: angalau asilimia 20 ya kaya hukosa kabisa chakula; angalau asilimia 30 ya watoto hukumbwa na utapiamlo mkali; na angalau watu wawili kati ya kila 10,000 hufariki kila siku kutokana na njaa na athari zake.
Ripoti imeongeza kuwa kufikia mwishoni mwa Septemba, zaidi ya watu 640,000, takriban asilimia 30 ya wakazi wote wa Gaza, wanatarajiwa kukabiliwa na viwango vya juu kabisa vya ukosefu wa chakula, huku wengine zaidi ya milioni 1.14 wakikumbwa na viwango vya dharura. Hali hii imetokana na takribani asilimia 98 ya mashamba ya eneo hilo kuharibiwa au kutofikika.