28/07/2025
Maisha⁉️
Maisha ya mwanadamu yamejaa mabadiliko yasiyotarajiwa. Kuna nyakati ambazo tunafanikiwa kupata, tunasherehekea lakini pia zipo nyakati ambazo tunapoteza, tunavunjika moyo au kukosa tunachotamani. Katika hali zote hizi ni muhimu sana kuufundisha moyo wako kuridhika. Kuridhika hakumaanishi kukata tamaa au kuacha kujaribu bali ni kuamua kuwa na amani ya ndani hata unapokosa kile ulichokitarajia.
Hali ya kupata au kupoteza siyo lazima iwe ishara ya baraka au laana. Mara nyingine kupoteza jambo fulani ni njia ya Mungu kukuondoa mahali pa hatari au kukuandaa kwa jambo bora zaidi. Hata unapopata sio kila kitu ulichokipata ni salama au cha kudumu, huenda kingekudhuru k**a moyo wako usingekuwa tayari.
Kwa hiyo kuufundisha moyo kuridhika ni hatua ya hekima. Ni kujenga uvumilivu, imani na utulivu wa ndani. Ni kukubali kwamba maisha siyo ya mstari mmoja bali ni mchanganyiko wa furaha na huzuni, mafanikio na changamoto.
Na ni katika kuridhika huko ndipo mtu hupata usalama wa kweli wa nafsi, usalama wa kutoyumbishwa na hali bali kusimama imara kwa sababu amani yako haitegemei kile unacho, bali msimamo wa moyo wako mbele ya kila hali.