01/08/2025
WAGOMBEA CCM MAFINGA, WAJIPAMBANUA KWA SERA THABITI........
Katika kuelekea upigaji wa kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kumpata Mgombea wa nafasi ya ubunge jimbo la Mafinga Mjini, Wagombea mbalimbali wamejitokeza kujinadi mbele ya wajumbe wa chama hicho, huku wakipambanisha sera na maono yao kwa ajili ya kuleta maendeleo ndani ya jimbo hilo.
Wagombea wa nafasi hiyo ya Ubunge katika jimbo hilo, Julai 31, 2025 wamekutana na wajumbe wa Kata ya Boma, Kata ya Upendo na Kata ya Wambi, ambapo Mratibu wa Kampeni za ubunge kura za maoni (CCM) Maines Kiwelu ambaye pia ni Mjumbe wa kamati ya siasa wilaya ya Mufindi amewasihi wajumbe kutafakari kwa makini sera zilizotolewa na wagombea katika kufanya maamuzi na kuwataka waache makundi.
Akizungumza katika nyakati tofauti na wajumbe wa kata ya Boma na Upendo, mbunge anayemeliza muda wake (anayetetea) nafasi hiyo ya ubunge ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato David Chumi ameeleza mafanikio na dhamira yake ya dhati ya kuendelea kushirikiana na wana Mafinga katika nafasi hiyo, akiweka wazi dhana yake ya kazi zinaongea.
Mgombea Mwingine wa nafasi hiyo ya ubunge ndani ya CCM ni Agrey Tonga ambaye amewaahidi mapinduzi ya maendeleo iwapo watampa ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho.
Wengine ni Dickson Nathan Lutevele, Mendrad Kigola na Dkt. Bazil Lwisijo Tweve ambao wameomba ridhaa kwa wajumbe huku wakieleza vipaumbele mbalimbali iwapo wakiaminiwa.